Thursday 18 May 2017

IMF YASIFU UCHUMI WA TANZANIA


SHIRIKA la Fedha la Kimataifa (IMF), limesema hali ya uchumi wa  Tanzania inaridhisha na ili kufikia uchumi wa kati, ni muhimu kuzingatia utulivu katika mfumuko wa bei kwa kuhakikisha unakuwa endelevu na kuondoa changamoto zinazoweza kusababisha mdororo wa uchumi.

Changamoto hizo zimetajwa kuwa ni kuyumba kwa uchumi kutokana na mfumuko wa bei, kutokuwepo kwa vichocheo vya uwekezaji, amani na utulivu, vitu ambavyo vinaweza kusababisha kutofikia Malengo ya Maendeleo ya mwaka 2020 hadi 2025.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Tao Zhang wakati akifungua mkutano wa wadau hao uliofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Zhang alisema ili kufikia uchumi wa kati, ni muhimu kuzingatia matakwa ya maendeleo endelevu kwa kuhakikisha kunakuwa na utulivu katika mfumuko wa bei.

Alisema hatua ya Rais Dk. John Magufuli kuimarisha ukusanyaji kodi na kupiga vita rushwa, itachochea sekta ya uchumi kukua kwa kasi, hivyo ni muhimu kuwa na taasisi imara ya ukusanyaji mapato na kuimarisha sekta ya biashara.

Alisema IMF itahakikisha inasimamia utulivu wa hali ya kiuchumi nchini kwa kushauri fursa za mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta binafsi.

“Tanzania ni kati ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambazo zinahitaji nguvu kubwa kuhimili utulivu wa kiuchumi. Ili kufikia lengo pamoja na mafanikio yaliyopo, sekta binafsi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya miaka mitano, hivyo ni muhimu kila mwenye uhitaji wa kuwekeza katika sekta za kiuchumi akapewa fursa,”alisema.

Alisema uwazi katika sera za uwekezaji ni muhimu ili kuondoa migogoro  katika sekta hiyo na kuwepo uelewa mpana wa masharti ya uwekezaji kwa kila mmoja kuweza kunufaika.

Alisema umuhimu wa kuwa na sera zisizobadilika mara kwa mara, utawafanya wawekezaji kuondoa hofu ya kukiukwa kwa mikataba ya uwekezaji hivyo kuwa na uhakika wa mitaji yao.

Zhang alisema uimarishaji wa vichocheo vya uchumi, ikiwemo kuwepo kwa miundombinu ya ukakika katika sekta ya usafirishaji kama vile umeme, barabara na huduma za kijamii, vitawafanya wawekezaji hao kuvutiwa kuwepo nchini.

“Ni lazima serikali ikubali kurudisha faida za uchumi kwa jamii kwa kuboresha sekta muhimu za huduma za kijamii, ikiwemo sekta ya usafirishaji,umeme huduma za kifedha ili kuwa na mazingira rafiki ya uwekezaji,”alisema.

Kwa upande wake, Gavana wa  Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benno Ndullu, alisema katika kikao hicho, wadau watahakikisha ziara ya Zhang inakuwa chachu katika maendeleo ya kiuchumi kwa kuongeza ushirikano wa kisekta.

No comments:

Post a Comment