Thursday 18 May 2017

JPM KUONGOZA MKUTANO WA 18 EAC


RAIS Dk. John Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya  Afrika Mashariki (EAC), Mei 20, mwaka huu, anatarajia kuongoza mkutano wa 18 wa nchi wanachama wa jumuia hiyo.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema mkutano huo utahudhuriwa na wakuu wa nchi zote sita wanachama.

Makonda alisema kufuatia ugeni huo mkubwa, Tanzania itaanza kuwapokea viongozi kuanzia Mei 19  hadi 20, mwaka huu. Alisema ugeni huo unatarajiwa kuondoka nchini Mei 21, mwaka huu.

“Ni mkutano wa siku moja na huu ni mkutano wa kawaida  wa EAC, hasa ikizingatiwa kwamba, Rais Dk. Magufuli ndiye Mwenyekiti wa Jumuia,”alisema Makonda.

Alisema pamoja na masuala nyeti, ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo, hii ni fursa nzuri kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, hususan kibiashara.

“Ni ugeni  mkubwa  wa watu wengi, ambao tunaamini watahitaji  kula, kulala  na kutumia vyombo vyote vya usafiri na pia kununua bidhaa zetu,”alisema Makonda.

Aliongeza: “Ninawaomba  wakazi wote wa mkoa wa Dar es Salaam, kuendeleza utamaduni wetu wa ukarimu kwa wageni, kudumisha amani na utulivu kwa wageni hawa.”

No comments:

Post a Comment