Tuesday 8 September 2015

DK MWAKYEMBE AMLIPUA KUBENEA






NA SOLOMON MWANSELE, KYELA

MGOMBEA Ubunge wa jimbo la Kyela kwa tiketi ya CCM,Dk.Harrison Mwakyembe, amesema  amefurahishwa na hatua ya mwandishi wa habari, Said Kubenea, kujiiingiza jumla kwenye siasa na kuwania ubunge.

Kubenea anagombea ubunge wa jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA, na atapambana na mgombea anayeipeperusha bendera ya CCM, Didas Massaburi.

Amesema hatua hiyo ni nzuri  na ana hakika kuwa kamwe Kubenea hawezi kufua dafu na kushinda mbele ya Massaburi.
Alisema ni wazi kuwa baada ya kushindwa kwenye kinyang’anyiro hicho, Kubenea ataanza kuandika vizuri habari zake.

Dk. Mwakyembe aliyasema hayo jana, wakati wa uzinduzi wa kampeni za jimbo la Kyela, ambapo mgeni rasmi alikuwa mmoja wa wajumbe walipo kwenye Kamati ya Kitaifa ya kampeni za CCM, Makongoro Nyerere.

“Nafurahi kuona watu kama kina Kubenea wanaingia kwenye siasa.Ni vyema ili waweze kupigwa ili wakaandike vizuri habari kwenye magazeti yao.Nina hakika yule (Kubenea) hawezi kushinda ubunge jimbo la Ubungo lile ni la Dk. Massaburi,” alisema Dk.Mwakyembe.

Katika hatua nyingine, Dk.Mwakyembe alimshangaa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA,Abraham Mwanyamaki, kutoa madai kuwa alitaka kuhongwa ili asijitokeze kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Dk.Mwakyembe alisema ni jambo la aibu kwa mwanaume kama Mwanyamaki, kusimama hadharani na kuzungumza uzushi kama huo kuwa kuna mtu anataka kumhonga ili asiwanie ubunge wakati anajijua wazi hana uwezo wa kutwaa jimbo hilo.

Dk.Mwakyembe, ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema mgombea huyo wa CHADEMA hana uwezo wa kutoa upinzani kwake, na kuwasihi wananchi wa Kyela watangulize mbele mambo ya maendeleo na siasa za kipuuzi waziweke nyuma kwani hazina maslahi kwa wana-Kyela.

Aidha, alisema hivi sasa maambukizi ya ukimwi wilayani humo yameshuka kutoka asilimia 17.2, mwaka 2005, hadi kufikia asilimia 9, hivyo kuwataka wananchi kuendeleza zaidi mapambano dhidi ya ugonjwa huo ili kuhakikisha maambukizi yanaendelea kushuka zaidi.

No comments:

Post a Comment