Tuesday 8 September 2015

BULEMBO AWATAKA WAANGALIZI WA UCHAGUZI MKUU KUMCHUNGUZA LOWASSA





NA LATIFA GANZEL, MVOMERO,
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi, Abdalah Bulembo, amewataka waangalizi wa uchaguzi kutoka nje ya nchi, waanze kumchunguza mgombea urais wa CHADEMA, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.
Bulembo amewataka waangalizi hao waanze kumchunguza Lowassa kwa madai kuwa anataka kuipasua nchi kwa misingi ya udini na ukabila.
Mwenyekiti huyo wa wazazi alisema hayo jana wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.John Magufuli, uliofanyika wilayani Mvomero.
Alisema amelazimika kusema hayo baada ya Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuph Makamba, kudai kuwa Lowassa alikwenda katika kanisa moja na kuomba viongozi wampigie debe kwa waumini ili wamchague.
Bulembo alisema mataifa yote ambayo yaliingiza siasa na udini, nchi zao zilitokea vurugu na zingine hazitawaliki.
“Nitawashangaa kama watu wa mataifa ya nje watamwacha Lowassa anayehatarisha amani ya nchi yetu,’’ alisema.
“Lowassa hana shida na kura za waumini wa dini zingine ni kwa nini anataka kuipasua nchi kwa udini?” Alihoji Bulembo.
Kwa upade wake, Makamba alisema Lowassa ni mwongo ambapo kabla ya kura za maoni alisema hawezi kuhama CCM na kwamba, asiyemtaka ahame.
“Ndani ya wiki mbili alibadili maneno haya mawili, ambapo wiki iliyofuata baada ya kuondolewa kugombea ndani ya Chama, alihama na kusema CCM sio baba yake wale mama yake bila kujali kuwa CCM ndio iliyomsomesha,” alisema.
Hata hivyo, alisema Dk. John Magufuli ana kila sifa ya kuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani.
Aliwataka Watanzania kumchagua Dk. Magufuli kwani ni kiongozi muadilifu na mwenye sifa.
Makamba alisema Lowassa wakati anaanza safari ya kugombea urais ndani ya Chama, aliwaahidi baadhi ya wapambe wake nafasi mbalimbali, ikiwemo ukuu wa wilaya na mikoa na alipohama Chama, watu hao walijua kuwa wamekosa nafasi hizo.
Alisema waliohama naye ni miongoni mwa aliowaahidi vyeo na kwamba, Lowassa hafai kuwa rais na haitatokea siku au mwaka akawa rais.
Makamba alisema alipokuwa Katibu Mkuu wa Chama, alichukua makapi ya upinzani akiwemo Tambwe Hizza, ambaye alisimama majukwaani na kuwatukana wapinzani.
Alisema baada ya kustaafu nafasi ya ukatibu mkuu, alipoingia katibu mkuu mwengine, Tambwe hakuwa na kazi tena hivyo, kutokana na njaa zake alirudi tena upinzani na kuanza kumtukana.

No comments:

Post a Comment