Tuesday 8 September 2015

KAMPENI HIZI SASA NI ZA HATARI, LOWASSA AOMBA KURA KANISANI, ATAKA RAIS WA AWAMU YA TANO AWE MLUTHERI, MAGUFULI AONYA UBAGUZI WA DINI USIPEWE NAFASI





NA WAANDISHI WETU
KAMBI ya UKAWA imeanza kuona dalili za kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao na sasa imemua kuingiza siasa kanisani.
Kutokana na hali hiyo, mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa na wapambe wake wameanza kuweweseka na kuifagilia CCM ikiwemo kwenye mikutano yao ya kampeni.
Katika tukio linaloweza kuitwa ni baya kujitokeza kwenye duru za siasa, juzi akiwa kanisani mjini Tabora, Lowassa aliwahubiria waumini wa dini yake siasa badala ya neno la Mungu.
"Naomba mniombee, mniombee kweli kweli. Nyie Walutheri mna sababu ya kuomba zaidi, kwa sababu tangu nchi hii iumbwe, haijapata kutoa Rais Mlutheri. Mwalimu Nyerere alikuwa Mkatoliki, Rais (Benjamin) Mkapa alikuwa Mkatoliki. 

"Sasa nadhani Mungu atatuongoza ili nasi tuweze kuipata nafasi hiyo. Kwa hiyo naomba mniombee sana,” alisikika akisema Lowassa akiwa kanisani.
Alijipigia debe kuwa anastahili kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu ni Mkristo wa madhehebu ya Kilutheri, kanisa ambalo halijawahi kutoa Rais tangu taifa hili lilipoundwa.
Lowassa, akiwa katika Kanisa la Kilutheri la Tabora, alisema ingawa taifa la Tanzania limewahi kutawaliwa na marais wanne, hakuna Mlutheri aliyewahi kushika wadhifa huo. Kanisa hilo liko Tabora Mjini, jirani na hoteli maarufu ya Orion Tabora.
Mmoja wa waumini waliohudhuria ibada hiyo na ambaye alikerwa na siasa kuingizwa kanisani, alisema  kabla ya kuomba kura mwisho wa ibada,  Lowassa aliwauliza waumini kama kuna asiyemfahamu.
Tukio hilo limetawala mitandao ya kijamii na watumiaji wengine wa simu, ambapo video inayomuonyesha Lowassa akiomba kura kanisani ni ya sekunde zisizozidi 25 na chapuo hilo la kuomba kura kanisani lilimalizwa na pambio
Tangu Tanzania kupata uhuru wake, marais walioiongoza ni Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, ambaye anamalizia muda wake.
Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi hapa nchini, wagombea wa nafasi zote za kisiasa hawaruhusiwi kufanya kampeni katika nyumba za ibada au kufanya siasa zinazochochea ubaguzi wa aina yoyote.
Katika awamu zote za viongozi hao, wamekuwa mstari wa mbele kukemea aina zote za ubaguzi ukiwemo wa kidini.
MAGUFULI AKEMEA
UBAGUZI WA KIDINI
Kutoka Turiani, Selina Wilson, anaripoti kuwa Watanzania wametakiwa kutokubali kugawanywa kwa misingi  ya dini, badala yake watangulize Utanzania kwa kuwa ndio kitu kinachowaunganisha
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, alisema hayo katika maeneo tofauti ya Wilaya za Mvomero na Kilindi, katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Magufuli aliwataka kuwa makini na watu wanaofanya siasa kwa misingi ya udini kwa kuwa ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
"Ndugu zangu hakuna kitu muhimu kama amani ya nchi yetu. Tuitunze amani. Tusibaguane kwa misingi yoyote ile," alisema Dk. Magufuli.
Alisema ana dhamira ya kuwaunganisha Watanzania wote na ndio maana anaomba kura kwa wananchi wa vyama vyote na watu wa dini zote.
"Watu tunazaliwa na mama zetu. Tukiwa kwenye matumbo ya mama kule hakuna vyama, wote ni binadamu. Inawezekana baba CCM, mama CHADEMA. Mapenzi hayana chama," alisema.
Dk. Magufuli alisema inawezekana baba akawa Muislam na mama Mkristo, hivyo ubinadamu hauna dini na kwa hiyo Watanzania wanapaswa kujenga umoja na mshikamano.
MAKAMBA APIGILIA MSUMARI
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mjini Turiani, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, aliwataka wananchi kuwa macho na wanasiasa wanaofanya kampeni kwa udini.
Makamba alisema kuna mgombea urais juzi alikuwa Tabora katika kanisa moja akiomba kura na kuwaeleza waumini kuwa sasa ni zamu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kutoa rais.
Alisema mgombea huyo aliwaambia waumini kwamba, madhehebu mengine na Waislamu walishawahi kupata rais, hivyo sasa ni zamu yao.
"Tusikubali kugawanywa kwa kuwa tunafanya uchaguzi wa rais anayefaa kuwa kiongozi wa watu. Mtu huyu hahitaji kura za injili," alisema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu, Abdallah Bulembo, aliwataka waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu kuanza na mgombea huyo kwa kuwa ameonyesha dhahiri kufanya kampeni za udini.
MALECELA NAYE AFUNGUKA
Wakati huo huo, Khadija Mussa anaripoti kuwa, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Bara, John Malecela, amesema mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli, atakiletea chama ushindi mnono.
Hata hivyo, aliwaponda wapinzani kwa kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki, hususan suala la kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Akizungumza na Uhuru jana, Malecela alisema Dk. Magufuli atakiletea Chama ushindi kutokana na kukubalika na wananchi pamoja na ahadi nzuri anazozitoa ambazo zinatekelezeka.
Alisema tangu aanze kampeni, Dk. Magufuli ameonyesha umahiri mkubwa wa kuelezea kilichomo katika ilani na mikakati yake mingine ya kuliinua taifa katika sekta mbalimbali, zikiwemo za elimu, afya, uchumi na kilimo.
“Muitikio wa wananchi katika mikutano yake ya kampeni imedhihirisha kwamba CCM bado inaendelea kupendwa na wananchi wana imani kubwa na Dk. Magufuli, hivyo suala la ushindi halina shaka,” alisema.
Hata hivyo, aliwataka viongozi na wana-CCM kutobweteka, badala yake kuendelea kufanya kampeni hata katika maeneo ambayo tayari Dk. Magufuli ameshapita ili kuzidi kuwashawishi wananchji kuipigia kura CCM.
Pia, alisema ni vema kwa wananchi kujiweka tayari na kuhakikisha wanamchagua Dk. Magufuli siku ya kupiga kura itakapofika ili aweze kushirikiana nao katika kuliletea maendeo endelevu taifa na wananchi kwa ujumla.
Aidha, aliwataka wananchi kutokubali kudanganyika na ahadi zisizotekelezeka zinazotolewa na wapinzani, kwa sababu hazina tija.
Malecela alitolea mfano masuala mawili ya utoaji wa elimu bure katika ngazi zote na wananchi kutolipa kodi ahadi ambazo ni hewa kwa sababu hakuna nchi yoyote duniani iliyoweza kufanya hivyo, na kwamba hata nchi tajiri wananchi wake wanalipa kodi.
“Hata nchi tajiri duniani wananchi wake wanalipa kodi, mfano Norway ambayo iligundua mafuta tangu miaka ya 1970, wananchi wake wanalipa kodi, mapato ya kodi ndiyo yatakayoboresha maisha ya wananchi katika taifa husika,” alisema.

No comments:

Post a Comment