Tuesday 8 September 2015

MBATIA AIPASUA UKAWA




WILIUM PAUL, VUNJO
VYAMA vinavyounda UKAWA vinazidi kupasuka baada ya madiwani wa CHADEMA kunyimwa eneo la kukaa kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za chama cha NCCR-MAGEUZI uliofanyika juzi katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, ambaye ni mgombea ubunge wa jimbo hilo, James Mbatia, alizindua kampeni hizo katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Marangu (TTC), ambapo madiwani wa CHADEMA hawakutengewa eneo la kukaa wala hawakunadiwa.
Kitendo hicho kilitafsiriwa kuwa ni sawa na kuwadhalilisha madiwani hao.
Wakizungumza na Uhuru kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini, madiwani hao walisema licha ya vyama vinavyounda UKAWA kuweka makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja kwenye kila jimbo na kata, NCCR-MAGEUZI wameshindwa kutekeleza agizo hilo kwa kusimamisha wagombea wa udiwani katika kata zote za jimbo hilo.
Aidha, walisema kutokana na hali hiyo CHADEMA nao wamesimamisha madiwani kwenye kata zote za jimbo hilo.
Mmoja wa madiwani hao alisema ni vigumu kukubaliana na hali hiyo kutokana na wao kutumia gharama nyingi na kwamba katika jimbo hilo, CHADEMA ndicho chenye kukubalika zaidi hivyo ingekuwa vyema wangeachiwa nafasi za udiwani kutokana na wao kuwaachia ubunge.
Alisema licha ya kunyimwa sehemu ya kukaa kwenye mkutano huo na kushindwa kutambulishwa, wataendelea na msimamo wao hata kama wakipelekwa kwenye kamati ya maridhiano kama ilivyokuwa hapo awali, hakitabadilika chochote.
Kwa mujibu wa mgombea udiwani huyo, iwapo wagombea udiwani wa NCCR-MAGEUZI hawataondolewa na wao hawatakubali kujiengua na kuwaachia nafasi hizo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbatia alisema madiwani walipewa maelekezo na makao makuu ya vyama vyao kwa maandishi, yakieleza kuangalia vigezo vya nani anayekubalika, mtandao wa mtu, uchaguzi wa serikali za mitaa ulivyokuwa na sio kila mtu kulalamikia anayefaa.
Mbatia aliwataka wagombea wote wa UKAWA kuheshimu makubaliano ya kile walichosaini kwa kutekeleza na sio kila mgombea wa chama kung'ang'ania wakati wamekubaliana.
Katika mkutano huo, Uhuru ilishuhudia daladala zikipita maeneo ya Vunjo na kukusanya watu kwa ajili ya kuwapeka katika mkutano ili uonekane umejaa.

No comments:

Post a Comment