Sunday 13 September 2015

KIGOGO CHADEMA AREJEA CCM




Na Latifa Ganzel, Morogoro
ALIYEKUWA Meneja wa Kampeni wa mgombea udiwani kupitia CHADEMA, Amos Chacha wa Kata ya Mkundi, Jimbo la Morogoro Mjini, amejiunga na CCM.
Meneja kampeni huyo, ambaye pia alikuwa katibu, alisema hayo jana, wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea udiwani wa kata hiyo, Hilda John, zilizofanyika kwenye kata ya Mkundi, jimboni humo.
Chacha alisema anajutia muda aliopoteza akiwa huko, ambako hakuna maendeleo yoyote zaidi ya ugomvi wa wenyewe kwa wenyewe, ambao hauna faida kwa chama.
Alisema akiwa kijana aliyesomeshwa na serikali ya CCM tangu akiwa kidato cha kwanza hadi chuo na kupata shahada ya juu ya sheria, hana sababu ya kukisaliti chama hicho na kuendelea kubaki kwenye chama pinzani.
“Kuwafahamu viongozi waliokuwa imara, kaa nao.
Nilikakaa nao na ndipo nikatambua kuwa hawapo sawa, nikaamua kurudi, siwezi kumuuza Mwalimu Nyerere na kwenda chama kisichoniwezesha kwa chochote,” alisema Chacha.
Akinadi sera zake, mgombea udiwani wa kata hiyo, Hilda alisema akichaguliwa, atasogeza huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme, barabara, kusimamia ujenzi wa shule ya msingi na sekondari ya kata sambamba na huduma za afya.
Alisema ikiwa wananchi hao watamchagua, atahakikisha huduma hizo zinawafikia kwa wakati ili kuondoa umaskini kwa jamii hiyo unaorudisha nyuma maendeleo ya watu.
“Mkinichagua nitahakikisha tunapigana na maadui watatu wa maendeleo, ikiwemo umaskini, ujinga na maradhi na kufanya kata yetu kusonga mbele kwa kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na vikundi mbalimbali kimikopo,” alisema.
Naye Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Maulidi Chambilila, aliwaomba wakazi wa kata hiyo kuwachangua viongozi wa CCM kwa kuzingatia mafiga matatu ya urais, ubunge na udiwani ili kuifanya serikali na wananchi wake kuweza kupiga hatua kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment