Sunday 13 September 2015

BWEGE ASHITAKIWA KWA SAMIA


 Mke wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika leo katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi


 Mgombea Mwwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan akijadiliana jambo na Mama Salma Kikwete na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Mtopa, baada ya kuwasili kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika leo eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi

NA ABDALLAH MWERI, KILWA KUSINI
WAKAZI wa Kilwa Kusini wamemshitaki mbunge wa Jimbo hilo, Selemani Bungala 'Bwege' kwa mgombea mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan kuwa ni kiongozi mbabaishaji.
Wakazi hao walitoa malalamiko hayo katika mkutano wa kampeni wa mgombea huyo mwenza, uliofanyika jana kwenye Kijiji cha Mandawa, Kilwa Kusini.
Walisema Bwege amedhoofisha maendeleo ya Jimbo la Kilwa Kusini na wanajuta kumchagua katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2005.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mandawa, Mariamu Mbonde, alisema kuwa mbunge huyo ameshindwa kujenga vituo vya afya, zahanati na ujenzi wa mabweni ya shule za sekondari.
Alisema wanawake wa Kijiji cha Mandawa wamekuwa wakijifungua kwa taabu katika zahanati kwa kukosa dawa na Bwege amekuwa hana msaada kwao.
"Hapa Mandawa hali ni mbaya, hatuna huduma za vituo vya afya, tunapata shida. Nitafurahi kama CCM itashinda katika uchaguzi mkuu ujao," alisema Mariamu.
Awali, Mbunge wa CCM anayewania ubunge katika jimbo hilo, Hasnain Dewji, alisema wakazi wa Kilwa Kusini wamekuwa wakiishi kwa taabu baada ya kukosa huduma muhimu vikiwemo vituo vya afya na zahanati.
Pia, alisema Kilwa Kusini imekosa huduma muhimu kama shule na soko la ufuta ambapo wakulima wamekuwa wakipata shida ya kuuza mazao yao kwa bei bora.
"Soko letu la ufuta lina changamoto kubwa, wakulima wanapata shida sana na hakuna mtetezi wa kuwatetea. Mkinichagu kuwa mbunge wa Kilwa Kusini nitajenga soko, vituo vya afya, zahanati na ujenzi wa mabweni," alisema Dewji.
Alisema kuwa amejipanga vyema kuwaletea maendeleo wakazi wa Kilwa Kusini endapo watamchagua katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Kwa upande wake, Samia alisema serikali ya awamu ya tano italeta maendeleo katika Jimbo la Kilwa Kusini, ikiwa ni pamoja na kuchukua ombi la ujenzi wa barabara ya Kilwa- Liwale.
Samia, aliwataka wakazi wa Kilwa Kusini kumchagua Dewji kwa kuwa CCM inatekeleza ilani ya uchaguzi, hivyo Watanzania wasifanye kosa kuchagua chama cha upinzani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mwantumu Mahiza, aliwataka wakazi wa Kilwa Kusini kuichagua CCM katika uchaguzi huo ili wapate maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, Mahiza aliwatoa hofu wakazi wa Mkoa wa Lindi kuwa kuna kundi la watu wamejiandaa kufanya vurugu katika uchaguzi huo, ambapo alionya yeyote ambaye atafanya fujo atakiona.
"Mimi ndiye Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, nimesikia kuna watu wamejiandaa kufanya fujo siku ya uchaguzi, wasithubutu, watakiona, serikali imejipanga vizuri kudhibiti hali yoyote ya uhalifu," alisema Mahiza.
Kampeni za mgombea mwenza huyo zinaendelea kupamba moto, baada ya kuzinduliwa rasmi Agosti 22, mwaka huu. Bendera ya CCM inapeperushwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na mgombea mwenza Samia.

No comments:

Post a Comment