Wednesday 7 October 2015

KIFO CHA MTIKILA KILIPANGWA- DP






NA MWANDISHI WETU
MAMBO mazito yameendelea kuibuka kufuatia kifo cha mwanasiasa mahiri nchini, Mchungaji Christopher Mtikila, ambapo hivi sasa inadaiwa kifo chake kilipangwa.
Mchungaji Mtikila alifariki dunia juzi, kwa ajali ya gari, iliyotokea katika kijiji cha Msolwa, Chalinze, mkoani Pwani.
Wakati utata ukiendelea kutawala kifo cha Mtikila, Mchungaji Patrick Mgaya, ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo, ameibuka na kusema Mungu atalipa damu hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha DP (Tanganyika), Abdul Mluya, alisema chama hicho kimesikitishwa na kifo cha Mtikila na kwamba, kinaamini kuwa kifo chake kilipangwa.
Alisema chama kimepata mashaka makubwa na mazingira ya kifo cha mchungaji huyo wa Kanisa la Full Salvation.
Mluya alisema hayo jana nyumbani kwa Mtikila, Mikocheni B, Dar es Salaam na kuongeza kuwa wanalitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kufanya uchunguzi wa kina wa kifo hicho.
“Ajali ya Mtikila, chama chetu kinamashaka nayo, hivyo tunavitaka vyombo vya dola, likiwemo jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kifo hicho,” alisema.
Alisema Oktoba 2, mwaka huu, Mtikila aliondoka Dar es Salaam kwenda Njombe kwa ajili ya kufanya mikutano ya kampeni, lakini walipofika njiani gari lao liligonga gari lingine kwa nyuma.
Mluya alisema mazingira ya ajali hiyo ilikuwa ya kutatanisha, kwani gari hilo lilionekana kulitegeshea gari alilopanda Mtikila.
Alisema Septemba 25-26, mwaka huu, Mtikila alifanya mkutano Bunda Mjini, ambapo alikuwa anafuatiliwa.
Mluya alisema kutokana na hali hiyo, walimuamisha Mtikila hoteli aliyofikia na kumpeleka kwingine, lakini kutokana na mazingira yaliyokuwepo, waliamua kumpeleka Mwanza.
Alisema wakati wanaenda Mwanza, walipofika Serengeti, kulikuwa na gari linawafuatilia, lakini walifika Mwanza salama.
Mluya alisema siku hiyo Mtikila alilala Mwanza na  asubuhi alikuwa na mahojiano katika kituo kimoja cha televisheni kilichoko Mwanza.
Alisema kutokana na mambo mbalimbali aliyokuwa anayaibua Mtikila hivi karibuni, alikuwa anafuatiliwa, hivyo hata kifo chake hawana imani nacho na kwamba kinaweza kuwa cha kupangwa.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema muda mfupi baada ya ajali ya Mtikila, kulikuwa na picha kwenye mitandao ya kijamii na mpaka sasa aliyezipiga hafahamiki.
Alisema picha hizo zimeongeza hofu, kwani ziliwekwa kwenye mtandao muda mfupi baada ya ajali na kwamba huyo aliyeziweka alikuwa sehemu gani wakati ajali inatokea.
Mluya alisema DP, wataendelea kuenzi matendo yake na mapambano aliyokuwa akifanya Mchungaji Mtikila.

MCHUNGAJI  MGAYA  AIBUKA
Mmoja ya watu waliopata ajali na Mtikila, Mchungaji Mgaya, alisema walikuwa kwenye mkutano wa kampeni Njombe, lakini wakati mkutano ukiendelea, zilikuja pikipiki mbili zikiwa na bendera za vyama viwili tofauti.
“Hizi pikipiki zilipita wakati mkutano ukiendelea zikiwa na bendera za vyama viwili tofauti ambavyo hakuzitaja.
“Bendera hizo nitazitaja siku nikiitwa na Mkurugenzi wa Upelezi wa Makosa ya Jinai, DCI  Diwani Athumani,” alisema Mgaya.
Alisema wakati wanatoka kwenye mkutano Njombe, walipofika Mafinga walikutana na gari aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa na rangi ya kijivu na muda wote lilikuwa likiwafuatilia.
Mgaya alisema wakati wanaendelea na safari, wakiwa Mikumi, Mchungaji Mtikila alitaka kujisaidia, hivyo wasisima.
Alisema wakiwa katika eneo la Mikumi, mara gari hilo likapita kwa spidi kubwa na muda huo gari lao likaondoka eneo hilo.
Mgaya alisema walianza safari, lakini dereva wao alikuwa anakimbiza gari kwa kasi licha ya kuonywa mara kadhaa na Mtikila kuwa asikimbize, lakini aligoma kupunguza mwendo.
“Yule dereva alidai anataka awahi kufika Chalinze, ili amkabidhi gari dereva mwingine atulete Dar es Salaam,” alisema.
Alisema walipofika eneo la Mdaula waliioona tena ile Cruiser ikiwa mbele kwa umbali wa mita 20, ambapo dereva wao alikuwa akilikimbiza.
“Tulipofika eneo la ajali, ile gari ilikuwa mbele yetu pembeni kulikuwa na lori, lakini wakati hiyo cruiser, ikijaribu kulipita lori, mbele kukatokea lori lingine.
“Nilidhani lori na cruiser litagongana uso kwa uso, lakini cha kushangaza sikujua ilipitaje na ndipo tukaingia sisi, tukajikuta gari letu lipo kwenye msingi,” alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa simu ya Mtikila haikuonekana pamoja na kuitafuta kwa muda mrefu baada ya ajali.
Mgaya alisema ni lazima Mwenyezi Mungu atalipa damu ya Mtikila.
Mwili wa Mchungaji Mtikila utaagwa leo katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam na baadaye utasafirishwa kwenda Ludewa kwa maziko.
000

No comments:

Post a Comment