Saturday, 17 October 2015

MAGUFULI AITEKA ZANZIBAR



NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli, amemaliza ziara ya kampeni Zanzibar na kuweka historia kuwa kiongozi aliyekusanya wananchi wengi hadi sasa katika kampeni za mwaka huu.
Mkutano wa mgombea huyo ambao ulifanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja mjini hapa, ulihudhuriwa na umati wa wananchi wa Zanzibar bila ya kujali vyama vyao vya siasa.
Dk. Magufuli ambaye juzi alifanya mkutano kama huo Pemba, amekuwa kivutio kwa wananchi wa Zanzibar ambapo kabla ya kuja kwake, wananchi wengi walikuwa wakiulizia mara kwa mara ratiba ya kampeni ya kiongozi huyo visiwani hapa.
Viwanja vya Mnazi Mmoja vilianza kujaa watu tangu saa sita mchana na kufanya barabara za eneo hilo kufungwa mapema tangu saa tano.
Katika hotuba yake, Dk. Magufuli aliwahakikishia wa Zanzibar kuwa akichaguliwa atakuwa Rais wa Watazania wote na kwamba amepata imani kubwa kutoka kuwa wananchi wa Zanzibar watamchagua kutokana na mapokezi yao makubwa.
“Nimesimama hapa kuomba kura. Nina imani na ninyi kwa kuwa mimi nimedhamiria kuwatumikia wananchi wa Tanzania bila ubaguzi,” alisema.
Aliwaeleza wananchi hao ambao walikuwa wakikatisha hotuba yake mara kwa mara kuwa alifurahishwa na walivyompokea tangu kuwasilisi kwake Zanzibar na watu wa vyama vyote walivyokuwa na hamu ya kumwona na kumsikiliza.
Dk. Magufuli aliahidi kupambana na rushwa na vitendo vya kiharamia kama vya uvunaji maliasili mfano uvuvi haramu katika bahari kuu kwa kuimarisha ulinzi wa bahari.
“Hapa ni kazi tu, nitawashughulikia mafisadi wote nikiingia madarakani ndiyo maana nilipopitishwa tu na Chama kugombea nafasi hii, mafisadi wote waliondoka CCM wenyewe,” alisema.
Mgombea huyo wa CCM alisisitiza umuhimu wa kuendeleza amani na utulivu nchini Tanzania  iendelee kuwa tulivu na kukaribisha wageni zaidi wakiwemo watalii ambao wanaingiza pato kubwa kwa taifa.
“Pasipo amani hakuna anayeweza kufungua duka, hakuna mtalii atakayekuja kutembelea Tanzania wala Zanzibar, hakuna mtu atakayekuja kujifunza historia ya Zanzibar ambayo inatajika ulimwenguni kote,” aliongeza Dk. Magufuli.
Aliahidi kushirikiana na Dk. Shein kuhakikishia amani na utulivu wa nchi unaendelea kuwepo nchini ili wananchi waweze kuendelea na shughuliza za kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake, mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema Zanzibar  na Tanzania bado zinastahili kuongozwa na viongozi kutoka CCM.
Shein ameuambia umati wa wananchi waliohudhuria kuwa CCM hakina mbadala nchini Tanzania na kwamba wagombea wengine katika uchaguzi mkuu watabaki kuwa wasindikizaji.
Dk. Shein aliahidi wakichaguliwa atashirikiana na kushauriana na Dk. Magufuli katika kuongoza Tanzania kama wanavyofanya sasa yeye na Rais Jakaya Kikwete na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa moja yenye amani na utulivu na kuendeleza Muungano wake.
Aliwataka wananchi kumchagua Dk. Magufuli ili awe Rais wa Tanzania na kwamba wakimchagua atakuwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.
“Mkimchagua Dk. Magufuli atakuwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, hivyo atatuhakikishia ulinzi wa nchi yetu na Muungano wetu,” alisema.
Alimsifu Dk. Magufuli kuwa kiongozi mwenye sifa zote zinazostahili kuongoza Tanzania na kuwa chini ya uongozi wake, Tanzania itaendelea kuwa salama salimini.
Aliwaleza wananchi kuwa Dk. Magufuli amekuwa waziri muda mrefu akiongoza wizara mbalimbali, hivyo ana uzoefu mkubwa wa uongozi serikalini na anaijua vyema serikali.
“Ni kiongozi mchapakazi. Uchapakazi  wake unafanana na tabia yake ya kupenda kwake kazi na anapenda ushirikiano na wenzake na sisi tunaamini huyu ndiye Rais wetu ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Dk. Shein alisema huku akishangiliwa na umati wa watu.
Aliongeza kuwa Dk. Magufuli ni muumini mzuri wa Muungano na anaujua vyema na kwamba amefanya kazi nzuri kuimarisha Muungano huo wakati akitekeleza majikumu yake aliyokuwa nayo.

No comments:

Post a Comment