Saturday, 17 October 2015

DK. SHEIN ATOA UJUMBE MZITO


NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi na wana CCM kuitumia vyema haki yao ya msingi ya kupiga kura Jumapili ijayo na kuwataka baada ya kumaliza kupiga kura, warudi nyumbani.
Amesema kwa mujibu wa Sheria za Tume ya Uchaguzi (ZEC) chombo chenye mamlaka ya kulinda kura ni tume kwa kushirikiana na vyombo vya dola.
Amewataka wananchi hususan vijana kutokubali kutumiliwa na watu wachache katika kuvuruga amani.
Dk. Shein alitoa rai hiyo jana wakati wa  uzinduzi wa tawi jipya la CCM la Mombasa Kwamchina, Dimani, Mkoa wa Magharibi Kichama, katika Jimbo la Kiembesamaki Zanzibar.
“Wananchi baada ya kumaliza kupiga kura rudini nyumbani na kusubiri kutangaziwa mshindi kwa kuwa ulinzi wa kisheria wa kura ni wa vyombo vya kisheria vilivyowekwa maalumu,” alisema.
Dk. Shein aliwahakikishia wana CCM kuwa atarudi Ikulu baada ya kura nyingi watakazompa  kutokana na kumkubali na kuzikubali sera za CCM.
Aidha, alimpongeza  Balozi Seif Ali Iddi, kwa kufanikisha kupatikana kwa kiwanja hicho na wana CCM wote waliowezesha ujenzi huo na kueleza kuwa hizi ni jitihada zake na zile za wana CCM za kukilinda, kukitetea na juhudi za serikali.
Alisifu hatua za kujitolea ndani ya  CCM ambazo juhudi hizo zilianzwa na mwasisi wa ASP, Mzee Abeid Karume, na kusema CCM ina kila sababu ya kufanya juhudi kutokana na historia yake kwa kuwa ndicho Chama  chenye historia ya ukombozi wa Zanzibar na kwamwe vyama vingine haviwezi kulingana na CCM.
Alisema viongozi wa CCM ni mahiri na wana uwezo wa kuongoza dola, ndiyo Zanzibar imeweza kupata mafanikio kutokana na uongozi wa CCM na kuwasisitiza wanaCCM kuendeleza wajibu wao, wakitumikie chama na Serikali yao.
Akizungumzia ujenzi huo, Dk. Shein alisema  unaenda sambamba na mradi wa CCM wa kumarisha Chama  na kutolea mfano wa kuzinduliwa kwa jengo jipya la CCM huko Dodoma Julai, mwaka huu, ujenzi wa jengo la UVCCM  lenye ghorofa 32 lililojengwa  Dar es Salaam.
Alipongeza azma ya tawi hilo ya kujenga maduka, mafunzo ya kompyuta, ushoni na ukodishwaji wa ukumbi wa mkutano,kuwaenzi wajasiriamali, shughuli za kijamii na kuwataka kuongeza kasi katika mipango hiyo kwa lengo la kuimarisha maslahi ya wana CCM wa tawi hilo.
 Dk. Shein aliwataka vijana kutokubali kupotoshwa na watu wasioitakia mema nchi yao ambao wako tayari kufanya lolote kwa ajili ya kulinda maslahi yao binafsi, bila ya kujali hali na maisha ya wengine.
Mbali na hayo, Dk. Shein alisema  matumaini yake kuwa tawi hilo litatoa elimu kwa CCM, na kuwataka vijana kujitokeza kwenda kupokea elimu ya itikadi na kwamba mafunzo ya itikadi ndiyo wanayoyafanya vijana katika nchi nyingine kuwa na moyo wa kizalendo na uchungu wa nchi yao.
Alisema siri kubwa  ya maendeleo ya nchi zinazoendelea ni mafanikio waliyoyapata katika kuwakuza vijana wao wakiwa na mapenzi na moyo wa kizalendo kwa nchi zao popote walipo.
Awali, Mwenyekiti wa ujenzi wa Tawi hilo, Ahmada Yahya Abdulwakil, alisema tawi hilo ni miongoni mwa matawi ya CCM yaliyomo katika Mkoa wa Magharibi Wilaya ya Dimani kichama, Jimbo la Kiembesamaki.
Alisema kuwa chimbuko la Tawi hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya katiba ya CCM Ibara ya 31 (2) kinachosema kuwa Tawi litafunguliwa tu iwapo mahala hapo panapohusika kuwa na wanachama wanasiopungua 50 na wasiozidi 600.
Katika ujenzi huo wanachama mbalimbali wa CCM walichagia akiwemo Dk. Shein  ambaye alitoa sh. milioni 17 ambazo zilisaidia kumalizia ujenzi wa Tawi hilo na Balozi  IddI ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alitoa  sh. milioni 5.8 na sh. milioni nne kwa ajili ya kununulia mbao za kuezekea.
Ahmada alisema kuwa hadi kumalizika kwa jengo hilo jumla ya sh.79,340,000 zimetumika.

No comments:

Post a Comment