Saturday, 17 October 2015

WAONYWA KUCHAGUA VIONGOZI KWA USHABIKI


Na Ahmed Makongo, Bariadi
WATANZANIA wameshauriwa kuacha kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, kwa kufuata ushabiki wa kisiasa.
Badala yake wametakuwa kuwa makini kwa kusikiliza sera na llani za vyama vya wagombea hao, ili wachaguwe viongozi makini na ambao hawawezi kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
Aidha, wananchi pia wameombwa kutokuchagua viongozi wabadilifu wa mali za umma na wale ambao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya ufisadi, kwa kuwa wakiwachagua viongozi wa aina hiyo ni sawa na kuiweka nchi reheni.
Ushauri huo ulitolewa juzi na mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Bunda Mjini, Stephen Wasira, wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwenye maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani iliyofanyika kitaifa katika mkoa wa Simiyu.
Wasira alisema  katika uchaguzi mkuu ujao Watanzania wanapaswa kuwa makini na kuacha kuchagua viongozi kwa kufua ushabiki wa kisiasa, bali wawe makini ili kuwachagua viongozi wenye sifa, ili kutokuiweka reheni nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano.
Alisema kuwa Watanzania wanapaswa kusikiliza sera za wagombea wa vyama mbalimbali pamoja na kuzisoma Ilani za vyama vyao, ili kuona ni chama gani chenye ilani yenye manufaa kwa jamii, badala ya kufuata ushabiki wa kisiasa.
Alisema wananchi wanapaswa kutambuakuwa Ilani ya chama husika ni mkataba kati ya mwananchi na viongozi watakaochaguliwa, hivyo wananchi wanalo jukumu kubwa la kutambua viongozi wanaofaa kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo, ili wawaletee maendeleo endelevu.
“Watanzania wenzangu tusichaguwe viongozi kwa kufuata ushabiki wa kisiasa. Chaguweni viongozi waadilifu, wasio na kasoro au wabadilifu wa mali za umma,” alisema.
Akizungumzia Ilani ya CCM ambayo yeye alikuwa mwenyekiti wa kuandika rasmu yake alisema imeweka masuala muhimu yanayolenga makundi mbalimbali ya kijamii, kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wote bila kujali Itikadi za kisiasa.

No comments:

Post a Comment