Sunday, 11 October 2015

MSIWAPE KURA WAPINZANI- MWIGULU




WANANCHI  wa Jimbo  la Bumbuli  wilayani Lushoto, wametakiwa kutofanya makosa kwa kuchagua wagombea wa upinzani, badala yake wawape kura wagombea wa CCM kwani ndio wenye uwezo na dhamira ya dhati ya kuwatumikia.
Aidha, wamekumbushwa kuwa mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Bumbuli, January Makamba, ndiye mgombea sahihi na anuani ya maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Timu ya Ushindi ya CCM, Mwigulu Nchemba, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi January, aliofanyika juzi, ambapo alisema mwanasiasa huyo ni hazina  kubwa  ya Taifa.
Nchemba alisema mgombea huyo ameonyesha umahiri wake katika kubuni na kusimamia miradi yenye nia ya kuwakwamua wananchi katika matatizo, tofauti na wagombea wa vyama  vya upinzani.
“Kimsingi January anaelewa kwa kina matatizo, kero na changamoto zinazolikabili jimbo hilo huku akiwa na uwezo,  maarifa na juhudi za kuleta ufumbuzi kwa masuala yote bila  kupoteza wakati,” alisema Mwigulu.
Mwigulu, ambaye pia ni mgombea wa jimbo la Iramba  Mashariki kupitia CCM, alisema anamuheshimu sana January kutokana na uwezo mkubwa wa kiutendaji aliokuwa nao na kwamba, anamuunga mkono kwenye harakati zake.
“Mchungwa mmeupanda wenyewe, mkaulea sasa unaanza kutoa matunda, anakuja mtu anawaambia muukate mkanunue machungwa kwingine. Kataeni na huyo mtu anatakiwa kuadhibiwa kwa kunyimwa kura,” alisema.
Kwa upande wake, January aliwataka wapigakura wa Bumbuli kuwapigia kura wagombea wa CCM kuanzia kwa Dk. John Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM.
Alisema bado ana deni la kulipa kwa wakazi wa Bumbuli, ambao alisema kama sio wao, asingeweza kujulikana na kufika mahali alipo sasa.

No comments:

Post a Comment