Sunday, 11 October 2015

WARIOBA: NI MAGUFULI PEKEE



NA WILLIAM SHECHAMBO
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema mapambano ya rushwa nchini si kazi ya Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pekee, bali uwepo wa kiongozi makini, msafi kama Dk. John Magufuli, akisaidiana na waadilifu wengine. 

Jaji Warioba, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, amesema Dk. Magufuli ni mtu sahihi wa kumkabidhi kazi ya kutokomeza rushwa hapa nchini kwakuwa ana maadili, hakutumia fedha wala kuwa na makundi kwenye mchakato wa kuomba nafasi ya kugombea urais ndani ya CCM na hana urafiki na matajiri.

“Mtu ambaye ana marafiki wengi matajiri si mtu sahihi na hafai kuongoza nchi kama Tanzania, ambayo kwa sasa inapigana kutokomeza rushwa, mtu anayetumia fedha kwenye kila kitu hafai. CCM wamefanya kazi nzuri kumpata Dk. Magufuli ataweza,” alisema Jaji Warioba.

Aidha, alisema mwanasiasa anayesimama jukwaani kusema viongozi wakuu wa serikali za awamu zilizotangulia tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi hii hawakufanya lolote la manufaa kwa taifa, anawadanganya Watanzania, hana fadhila.

Amesema mafanikio ya jitihada zilizofanywa na viongozi wa awamu zote nne yanaonekana wazi na kwamba Tanzania isingefika ilipo sasa bila kuwepo kwa mchango mkubwa wa viongozi hao, ambao pia kutokana na uchapakazi wao walipewa heshima kubwa ndani ya nchi na kimataifa.

Jaji Warioba alisema moja ya mambo makubwa waliyoyafanya marais wa awamu zote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo mpaka kesho litaendelea kuliletea taifa sifa kimataifa kama wachache wanaoonyesha dalili ya kulivuruga watashindwa ni umoja.

Akizungumza jana kwenye mahojiano maalumu na kituo cha televisheni cha Star kilichoko jijini Mwanza, Jaji Warioba alisema umoja, mshikamano ni jambo ambalo viongozi wa awamu zote wamelisimamia kwa uaminifu, hali iliyosababisha kuwepo kwa amani na kukwepa ukabila.

“Huwezi kufanya kitu chochote cha maendeleo kama hakuna amani, umoja ndio umetuletea amani na haijatokea tu, ni viongozi wetu ndio waliotulea kwenye misingi hii ya umoja, hivyo kutuletea maendeleo tunayoyaona sasa. Mwanasiasa anayesema hakuna kilichofanyika, hajitambui,” alisema.

Alisema yako mambo mengi ambayo Watanzania wanastahili kujivunia kwa kutembea kifua mbele duniani, lakini inashangaza anapotokea mtu ambaye cha kusikitisha zaidi anaufahamu wa mambo hayo, lakini kwa maslahi yake anajitoa ufahamu na kuilinganisha Tanganyika ya 1961 na Tanzania ya leo.

“Suala la elimu ambalo linapigiwa kelele sana kwenye majukwaa ya kisiasa, kama unakumbuka baada ya Uhuru, Mwalimu (Nyerere) kupitia TANU aliweka msisitizo mkubwa kwenye sekta ya elimu, vivyo hivyo awamu ya pili na tatu na sasa ya nne msisitizo umewekwa kwenye elimu ya msingi, kila mtoto aende shule, matunda yanaonekana.

“Shule za kata za sekondari zimetapakaa kila kona ya nchi licha ya kuwa na changamoto kadhaa, lakini jitihada zinaendelea kufanywa na serikali ikiwemo kuajiri walimu na kupeleka vitabu, watu wanayaona haya, ni kazi imefanyika,” alisema.

Aidha, alisema kwenye sekta ya afya, vifo vya watoto wanaokufa chini ya umri wa miaka mitano vimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na uwepo wa elimu ya uzazi, zahanati kwenye karibia kila kata, hospitali ambazo mpaka sasa zinaendelea kuwahudumia Watanzania kwa ubora wa hali ya juu kutokana na serikali kuwasomesha, kuwaajiri wataalamu wa afya kwa ajili ya wananchi.

Alisema alifanyakazi chini ya uongozi wa Mawaziri Wakuu akiwemo Marehemu Kawawa, Sokoine na Cleopa Msuya, ambao wote kwa nyakati tofauti walifanyakazi kubwa ya kuijenga Tanzania kwenye sekta zote, ikiwemo afya kiasi cha baadhi yao kupewa majina maalumu kutokana na uchapakazi wao.

“Kwa mfano Mzee Kawawa alifanya kazi kubwa sana kuijenga nchi yetu, mpaka akapewa jina ‘Simba wa vita’, ambalo lilivuma kote nchini na sote tulilikubali. Leo eti unasema hakufanya chochote na serikali yake. Inashangaza sana,” alisema Jaji Warioba.

Pamoja na hayo, Jaji Warioba alilaani kampeni za kikabila, kidini na kikanda zinazoendelea hapa nchini kwenye baadhi ya vyama vya siasa na kusema hizo ni dalili mbaya za kuleta nyufa kwenye umoja wa Watanzania uliojengwa kwa miaka mingi tangu kupatikana uhuru wa nchi hii.

Alisema siasa ilikuwepo, ipo na itaendelea kuwepo hivyo hakuna sababu Watanzania kuwa na uhasama kutokana na kutofautiana kiitikadi kwa kuwa hujenga chuki na umoja uliopo nchini unaweza kuvunjika kutokana na uwepo wa vitendo vya aina hiyo. 

No comments:

Post a Comment