NA KHADIJA MUSSA, KAHAMA
MJUMBE wa Kamati ya kampeni ya ushindi wa CCM, Christopher Ole Sendeka, amemponda mgombea ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, James Lembeli kwamba hana nyumba jimboni humo na analala nyumba za wageni.
Amesema hakuna mwakilishi wa wananchi, ambaye hana makazi ya uhakika kwenye eneo analoliongoza na kwamba, Lembeli hapaswi kupewa uongozi.
Amesema Lembeli amewalaghai wananchi kwa kujifanya ni kamanda wa kupambana na ufisadi na sasa amejiumbua mwenyewe kwa kuonyesha wazi kuwa ni mbabaishaji baada ya kujiunga na chama, ambacho mgombea wake wa urais ni Edward Lowassa, ni mtuhumiwa wa ufisadi.
Ole Sendeka aliyasema hayo jana, katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye jimbo la Kahama Mjini na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi ambapo, aliwataka wasimchague kwa kuwa ameshindwa kuwatumikia.
Alisema wananchi wa jimbo hilo lazima wawe makini na kukataa kuongozwa na kiongozi ambaye, kwa muda wa miaka 10 ya ubunge wake ameshindwa kuwa hata na nyumba, badala yake analala gesti, jambo ambalo linawawia vigumu kumuomba msaada pale wanapohitaji.
"Lembeli hafai kuchaguliwa tena ndugu zangu maana ni mbabaishaji. Awali alisema ana ugomvi na Mgeja na hawezi kukaa naye meza moja na alimlalamikia kuwa anatumiwa na Lowassa kummaliza jimboni, sasa naomba nikuulize haya mapenzi ya ghafla kati yake na Mgeja na Lowassa yametoka wapi?" Alihoji Sendeka.
Akizungumza kuhusu mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia alisema wataingia Ikulu bila ya kuwa na deni la wafanyabiashara, hivyo hawatakuwa na kazi ya kulipa fadhila, badala yake wataingia kwa ajili ya kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi.
Aliongeza kuwa tangu alipochukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais na hadi kupewa dhamana hiyo, hakuwahi kuomba ufadhili au kusaidiwa kiasi chochote cha fedha kutoka kwa wafanyabiashara, hivyo wanaotegemea hisani wataumbuka.
Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo, Jumanne Kishimba, alimuomba Samia atakapoingia madarakani kuwasaidia katika kutatua changamoto za sekta ya afya, ikiwemo upungufu wa vitanda vya kujifungulia na vifaa tiba.
Kishimba, alimshukia Lembeli kuwa kwa miaka 10 ameshindwa kusaidia hospitali ya wilaya ambayo ina vitanda vinane tu vya kujifungulia na inapokea kinamama zaidi ya 50 kwa siku, hivyo kusababisha baadhi yao kujifungulia katika vitanda vya kawaida.
Alisema wakati umefika kwa wananchi kuchagua kiongozi, ambaye atakuwa mwakilishi wa matatizo yao na aliyekuwa tayari kuwatumikia, hivyo aliwaomba wananchi hao kumchagua ili aweze kuwatumikia.
MAKONDA
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema wananchi hao hawana haja ya kuendelea kumchagua Lembeli kwa kuwa ameshindwa kuwaletea maendeleo katika kipindi chote cha uongozi wake.
Alisema Lembeli ni mpigadili, ambaye alikuwa anadanganya watu kuwa anauchukia ufisadi na sasa ameuonyesha umma baada ya kuungana na wenzake, hivyo hafai kuwa kiongozi, badala yake aliwaomba wananchi hao wamchague Kishimba awe mbunge wao na maendeleo watayaona.
SAMIA
Kwa upande wake, mgombea mwenza aliahidi kushughulikia kero mbalimbali za wananchi wa wilaya ya Kahama, ikiwa ni pamoja na kufufua upya bandari kavu ya Isaka, ambayo ilikuwa ni tegemeo kubwa kwa wananchi hao kiuchumi.
Alisema bandari kavu ya Isaka ilikuwa inatoa ajira nyingi kwa vijana, hivyo kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi na umasikini wa kipato, hivyo serikali ijayo imeweka mikakati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuifufua bandari hiyo.
Mbali na hayo, Samia aliahidi kumaliza tatizo la upungufu wa vitanda vya kujifungulia katika hospitali ya wilaya ya Kahama, kwa kupitia Ilani ambayo imeelekeza kuboresha huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kinamama kujifungua katika maeneo ambayo ni salama.
Alisema atahakikisha wanamaliza tatizo la vifo vya mama na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, kwa kuimarisha miundombinu ya hospitali na kuboresha huduma kwa kuongeza wataalamu, vifaa tiba na kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali, zahanati na vituo vya afya.
Samia aliwaomba wananchi hao kumchagua Dk Magufuli ili waweze kushirikiana naye katika kutatua kero zinazowakabili na wasithubutu kumchagua Lowassa kwa kuwa hana msimamo.
Alisema Lowassa usoni anaonekana UKAWA na moyoni ni CCM na juzi alidhihirisha hilo katika mkutano wake Tarime, baada ya kuomba wananchi wachague wagombea ubunge wa CCM.
No comments:
Post a Comment