Sunday, 11 October 2015

WATU 503,860 KUPIGAKURA ZANZIBAR


MWENYEKITI  wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha amesema jumla ya wapiga kura 503,860 wanatarajiwa kupigakura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Zanzibar.

Uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, utawachagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani,pamoja na uchaguzi mkuu wa rais wa Tanzania na wabunge.

Akitoa taarifa katika mkutano wa wadau wa uchaguzi mkuu jana, Jecha alisema watu hao wamepatikana baada ya tume hiyo kukamilisha zoezi la uendelezaji wa daftari la kudumu na kuzifanyia uchambuzi taarifa za wapigakura walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura.

Alisema katika mchakato huo uliofuatiwa na kugawiwa kwa shahada hizo kwa wapiga kura hao wiki iliyopita, jumla ya wapiga kura 7,743 wamefutwa baada ya kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.

“Kazi za uendelezaji wa daftari la kudumu la wapiga kura limekamilika kama moja ya hatua muhimu katika matayarisho ya uchaguzi na tume tayari tume imekamilisha uchapishaji wa daftari hilo ambalo tumeanza kulikabidhi kwa wagombea na baadae
litabandikwa katika vituo,” alisema Jecha.

Aliongeza kuwa zoezi la kuliweka hadharani daftari hilo litafanyika kuanzia Oktoba 18, mwaka huu, ili kutoa nafasi kwa wapigakura hao kujua vituo vya kupigia kura kwa lengo ka kupunguza msongamano siku ya kupiga kura.

Aidha, alisema katika uchaguzi huo, tume hiyo imepanga kuwa na maeneo 380 na vituo 1,580 vya kupigia kura ambapo kila kituo kinatarajiwa kuwa na wastani wa wapigakura 350.

Alizitaja shughuli nyingine zinazofanywa na ZEC kuelekea katika uchaguzi huo kuwa ni pamoja na uteuzi wa watendaji watakaosimamia zoezi hilo, kutoa mafunzo kwa watendaji hao na kutoa vibali kwa waangalizi wa ndani na nje wa uchaguzi huo.

Mbali na kazi hizo, alisema tume imeshaanza kupokea baadhi ya vifaa vitakavyotumika katika uchaguzi huo, ambapo karatasi za kura zinatarajiwa kuwasili nchini baadae wiki hii na kueleza kuwa vyama hivyo na wadau wengine wa uchaguzi wataalikwa kushuhudia zoezi hilo.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika maandalizi ya uchaguzi huo, bado tume inakabiliwa na changamoto za kisheria na kiutaratibu katika utekelezaji wa kazi zake.

“Kwa vile sheria ya uchaguzi ipo kimya kuhusu sifa za ukaazi za wakala wa kuhesabu kura, tume ya uchaguzi imelitolea ufafanuzi kuhusu suala hili na kwamba mgombea hafungiki kuweka wakala wa kuhesabia kura ambaye anaishi katika eneo hilo ilimradi awe ameruhusiwa na tume”, alisema Jecha.

Alivitaka vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo na wadau wengine wa uchaguzi huo kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya vyama vya siasa, miongozo na taratibu mbali mbali zilizowekwa na tume ili kuwa na
uchaguzi huru, haki na wa amani.

Wakiichangia taarifa hiyo, baadhi ya wadau hao kutoka vyama vya siasa, waliipongeza tume hiyo kwa hatua inazochukua za kuwapatia taarifa juu ya maendeleo ya maandalizi ya uchaguzi huo.

“Tunashukuru toka mmeanza matayarisho ya uchaguzi wa mwaka huu, mmekuwa mkitushirikisha, lakini hili la mgawanyo wa mipaka ya majimbo ni lazima mlichukulie hatua za haraka kwani uchaguzi unakaribia, lakini bado kuna tatizo la watu kutojua ni wapi watapiga kura”, alisema Suleiman Abdallah, Naibu Katibu wa chama cha NRA.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Uenezi wa TADEA, Yussuf Mchenga, aliitaka tume hiyo kuangalia uwezekano wa kupunguza ada za kugombea katika nafsi mbalimbali za uongozi ili kutanua wigo  wa watu wenye sifa za kugombea wafanye hivyo.

“Tofauti ya ada na ukubwa wa viwango vilivyopo kati ya ZEC na NEC vinatofautiana, jambo ambalo linaminya fursa ya kugombea kutokana na kukosekana kwa uwezo wa fedha”, alisema Mchenga akitolea mfano wa tofauti ya viwango vya ada ya kugombea urais wa Zanzibar na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akilitolea ufafanuzi jambo hilo, Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Abdulhakim Ameir Issa, alisema jambo hilo linatokana na sheria na kanuni za uchaguzi zilizopo, lakini tume yake italifanyia kazi.

No comments:

Post a Comment