Wednesday 7 October 2015

MTIKISIKO ARUSHA, DK MAGUFULI AWEKA REKODI NYINGINE MPYA

Msafara wa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ukiingia kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha
Umati  wa wananchi uliofurika kwenye mkutano wa kampeni wa Dk. Magufuli mjini Arusha
Dk. Magufuli akiwahutubia wananchi mjini Arusha
Dk. Magufuli akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiwahutubia wananchi wakati wa mkutano huo
Dk. Magufuli akishangiliwa na wananchi wakati msafara wake ulipokuwa ukiingia uwanjani
Mgombea ubunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka akihutubia wananchi
Dk. Magufuli akimtambulisha mgombea ubunge wa jimbo la Monduli, Namelok Sokoine
Dk. Magufuli akiweka shada la maua kwenye kaburi la Waziri Mkuu wa zamano, Edward Moringe Sokoine



NA CHARLES MGANGA, ARUSHA

MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amewahakikishia Watanzania kuwa uongozi wake utafuata nyayo za Hayati Moringe Sokoine.
 Amesema maslahi ya Watanzania, hasa wanyonge yatazingatiwa na kwamba hakutakuwa na nafasi kwa viongozi na watendaji wala rushwa.
Pia ameelezea kushangazwa na umati mkubwa uliojitokeza katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini hapa na kufananisha hali hiyo na mafuriko ya tsunami.
Amesema umati huo umemfurahisha na kudhihirisha ukweli kwamba, tayari Watanzania wameshakubali yeye ndiye rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
“Hakika Arusha mmefunika. Idadi kubwa ya watu kiasi hiki, hii haijapata kutokea… ni funga kazi kweli kweli.Mmenifurahisha sana.
“Kuna waliosema Arusha sitapata watu, wote hawa kila kona kweli, Watanzania wameamua kutaka mabadiliko na tayari nimeshashinda,” alisema Dk. Magufuli.

Aidha, Dk. Magufuli ambaye awali alifanya mikutano katika maeneo ya Mto wa Mbu, Monduli na Longido, aliwashukia watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuwataka kujiandaa kuondoka katika nafasi zao kutokana na tatizo la kukatika umeme kila wakati.

Alisema haiwezekani, umeme ukatike katika kipindi cha kampeni, huku akisema wanaodhani, wanafanya hivyo kwa ajili ya kumkomoa wanajidanganya.
Pia, alisema mawaziri wanaoshughulika na umeme wanapaswa kuajiangalia kwani, kukatika kwa umeme mara kwa mara kunasababisha umasikini kwa Watanzania.
“Haiwezekani kabisa umeme uwe unakatika kipindi hiki cha kampeni. Tatizo hili limeongezeka kwa kiasi kikubwa. Wanataka Watanzania wanichukie ama waichukie CCM… watu wa umeme wajiandae,” alisema huku akishangiliwa na umati wa watu.
Alisema kukatika kwa umeme kunaweza kuwa kunafanyika kwa sababu zisizo na msingi na zilizoegemea katika itikadi za kisiasa.

Hata hivyo, aliwataka Watanzania kuvumilia, kwani zimesalia siku 17 tu kabla ya uchaguzi, ambapo akichaguliwa atachukua hatua kali dhidi ya vitendo vya ukataji wa umeme wa hovyo.

Akizungumzia suala la ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Magufuli alisema serikali yake itaendelea kuimarisha uhusiano na nchi zinazoizunguka Tanzania.

Alisema kwa kufanya hivyo, kutaendelea kuwezesha mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia ambayo tayari umeshajengwa na awamu za serikali, zilizotangulia.

“Nitaendelea kuimarisha uhusiano wetu mzuri na nchi za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na zingine zilizo karibu.

“Kenya ni majirani zetu, tutaendeleza ushirikiano wetu wa kibiashara kama ilivyo sasa,” alisema Magufuli.

Pia, Dk. Magufuli aliwaambia watu waliobinafsishiwa viwanda, kuviendeleza kabla ya siku ya kuingia madarakani.

Alisema kitendo cha viwanda hivyo kutoendelezwa, kinawakosesha vijana ajira na kuinyima serikali mapato.

Alivitaja baadhi ya viwanda hivyo ni kile cha matairi cha General Tyre, ambacho kilisaidia vijana wengi kufanya kazi hapo.
na kiwanda cha nguo cha Kiltex, ambavyo amevitaka vianze kazi mara atakapoingia madarakani.

“Nimeshasema na narudia, waliobinafsishiwa viwanda na wameshindwa kuviendeleza wajiandae kuvirejesha ama kuviendeleza,” alisema.

Alisema wakishindwa kuviendeleza viwanda hivyo, atavirejesha serikalini kwa manufaa ya Watanzania wote.

Mgombea huyo wa CCM, alisema serikali yake inataka kujenga Tanzania mpya ya viwanda. Itajenga viwanda vikubwa vya kati na vidogo, kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa.

Alisema serikali yake inataka kufanya mabadiliko makubwa, hivyo amewataka wale wanaobeza, kuwapuuzwa.
Dk. Magufuli alisema anachoamini maendeleo hayana chama, udini, wala ukanda, jambo la msingi ni kuungana kufanikisha ndoto hiyo ya kuijenga Tanzania mpya.

“Nimekuwa nikisema, maendeleo hayana chama, dini wala ukanda. Jambo la msingi, tuungane kwa pamoja, tushirikiane na kushikamana kuyapata maendeleo,” aliongeza.

Dk. Magufuli alisisitiza kwamba wawekezaji kuzingatia masharti ya kuajiri Watanzania kwa asilimia fulani kinyume na wanavyofanya wawekezaji wengi kwa kuja na wafanyakazi wao.

Kuhusu utalii alisema ana mpango wa kuibadilisha Arusha, iwe kitovu cha utalii katika ukanda wa Afrika.

Alisema anashangazwa na umaarufu wa Arusha kutoweka, hivyo serikali yake inakusudia kurejesha hadhi hiyo iliyotoweka kwa muda mrefu sasa.

“Arusha ni mji wa utalii, lakini hadhi hiyo imetoweka kabisa kwa sababu zisizoeleweka, serikali yangu nitakayoiunda kuujenga upya mji wa Arusha uweze kuendelea kukuza sekta ya utalii wetu,” alisema Magufuli.

Dk. Magufuli alisema atahakikisha tatizo la maandamo ambalo lilikuwepo na kufanywa na watu wa upinzani mpaka kupoteza, amani kwa watalii, hali hiyo itarekebishwa na serikali yake.

“Maandamano yaliyokuwa yakifanyika mjini Arusha, yamekuwa yakiwaletea hofu watalii na hivyo kupunguza idadi ya watalii nchini. Serikali yangu italishughulikia hilo,” alisema.

Alisema si hayo tu, serikali atakayoiunda, imedhamiria kufanya mambo makubwa, jambo la msingi ni kurejesha amani na hadhi ya Arusha iliyopotea.

Dk. Magufuli aliwahakikishia watu waliovunjiwa nyumba zao kupisha ujenzi wa barabara jijini Arusha kuwa zimetengwa  sh. bilioni 22 kwa ajili ya kuwalipa kwa mujibu wa sheria.

“Hawa wala wasiwe na wasiwasi, fedha zimeshatengwa kwa ajili ya kuwalipa haki yao kwa mujibu wa sheria ya ardhi na ile ya mipango miji namba 4 na 5 ya mwaka 1999,” alisema Dk. Magufuli.

KUFUATA NYAYO ZA SOKOINE

Dk. Magufuli alisema anataka kufanya kazi kwa kufuata nyayo za Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Moringe Sokoine.

Alisema marehemu Sokoine alikuwa akipiga vita ufisadi, rushwa na uzembe na kwamba atahakikisha serikali yake itatatua matatizo ya Monduli.

Dk. Magufuli, ambaye kabla ya kuzungumza na wananchi wa Monduli, alizuru kaburi la Sokoine, alisema atahakikisha mabwawa ambayo yaliyobomoka, yanatengenezwa, ili kupunguza kero ya maji na  maeneo ya  kunyweshea mifugo.

"Sipendi mafisadi na siku zote nimekuwa mkweli kusimamia hilo... hata Sokoine alichukia hayo pamoja na watu kuonewa, nitafuata nyayo zake. Nitatengeneza haya kumuenzi Hayati Sokoine," alisema Dk. Magufuli.

Aidha alisema kwamba serikali yake itahakikisha hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa. Pia alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu wananchi wanaotishwa kuwa siku ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani na kusema ulinzi utaimarishwa, ili kila Mtanzania atimize haki yake ya kikatiba.

"Nasikia mnatishwa na baadhi ya watu…tunajua huo ni mkakati ili kuvuruga uchaguzi…jitokezeni kwa wingi na mkadhihirishe kwa kuipigia kura nyingi wagombea wa CCM," alisema Dk. Magufuli.

Aliongeza kusema ana uhakika hata kama kura zikipigwa leo, ataibuka mshindi katika nafasi anayogombea.
Alisema anajua wapinzani wamekuwa wakitoa fedha kwa wananchi, hivyo aliwataka wachukue, lakini wachague viongozi wa CCM.

"Hizo fedha chukueni, kuleni kwa sababu ni zenu, mafisadi waliwaibieni siku nyingi," alisema Dk. Magufuli.

KINANA: VIKAO VIFUTWE
Wakati akizungumza, Kinana aliishauri serikali ya Dk. Magufuli kufuta vikao vya watendaji, kwani vinachangia kukwamisha ufanisi na kuwahudumia watu kwa wakati.

Kinana alisema vikao hivyo ni vyema vikapunguzwa au kufutwa kabisa kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi katika kuongeza kasi ya maendeleo.

Dk. Magufuli ambaye tayari ameshafanya mikutano ya kampeni mikoa 21, ataendelea kuomba kura maeneo mengine ya jiji la Arusha, kabla ya kuingia Mkoa wa Kilimanjaro.

HUJUMA ZA  UKAWA  ZAKWAMA
Hujuma na mchezo mchafu uliopangwa na viongozi na wafuasi wa UKAWA dhidi ya mikutano ya Dk. Magufuli jana, zilishindwa kupambana na nguvu na hamasa ya wananchi.
Awali, viongozi wa UKAWA mkoani hapa walitekeleza maelekezo ya wakubwa wao kwa kuandaa vijana wa kumzomea Dk. Magufuli na msafara wake pamoja na kutangaza hali ya hatari ili kuwazuia wananchi wasihudhurie mkutano huo.
Pia, walikodisha vyumba kwenye hoteli nyingi jijini hapa kuzuia msafara huo usipate malazi pamoja na kutangaza kuwa mikutano ya Dk. Magufuli na wagombea wa CCM imefutwa.

Hata hivyo, mchezo mchafu huo ulibainika mapema na kudhibitiwa na mambo kwenda kama yalivyopangwa.


BENKI  MTO  WA MBU
Akiwa eneo la Mto wa Mbu, Dk. Magufuli alisema atahakikisha Benki ya CRDB inafungua tawi, ili wananchi wapate huduma za kifedha.
Alieleza masikitiko yake kwa viongozi waliokuwa wakiongoza Jimbo la Monduli kushindwa kuzungumza na benki ili kufungua matawi ya kuwahudumia wananchi.
Pia alimwomba Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kufungua ofisi katika eneo hilo, kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
"Nitaongea na viongozi wa taasisi na mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kufungua tawi kwa ajili ya huduma kwa wananchi,” alisema.

Aliwaomba wananchi kumchagua mgombea ubunge wa Monduli, Namelok Sokoine, ili awaletee maendeleo ya haraka.

Alisema Namelok ataendeleza yale ambayo Hayati Sokoine, aliyodhamiria kuyafanya enzi ya uhai wake.

Akiwa, Longido, Dk. Magufuli aliahidi serikali yake kutatua changamoto zilizopo ndani ya wilaya na jimbo hilo.

Moja kati ya ahadi hizo ni kuanzisha soko la mifugo, ambalo litainua kipato chao na kuahidi  kuwa serikali yake itakuwa karibu na wafugaji kwa kuwapa elimu na kuwawezesha kukopa.

Suala la mpango wa matumizi  bora ya ardhi, nalo  alisema litazingatiwa katika kipindi cha awamu ya tano ya serikali yake.

"Nitaimarisha mfuko wa maendeleo ya mifugo, ili wafugaji wafanye ufugaji wenye tija," alisema Dk. Magufuli.

Kabla ya Dk. Magufuli kupanda jukwaani, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwasalimia wananchi na kusema wale wenye mashaka na CCM, wanapoteza muda.

"Tayari ushindi ni wa Magufuli kwa sababu atatua kero za Watanzania," alisema Kinana.

Aliwaambia wananchi wa Longido kwamba Dk. Magufuli ni mwadilifu na  mchapakazi hodari.

No comments:

Post a Comment