Tuesday 17 November 2015

BUSARA ITUMIKE UZINDUZI WA BUNGE LA 11




Na Joseph Kulangwa
IJUMAA wiki hii, Rais Dk. John Magufuli anatarajiwa kuzindua Bunge la 11 la Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania kwa kulihutubia kama ilivyo ada kwa miaka yote uzinduzi wa Bunge jipya unapofanyika.
Ni wakati ambao Rais atatumia fursa hiyo adhimu kulitangazia Taifa nini anakusudia kulifanyia katika kipindi chake cha miaka mitano ya urais, baada ya Watanzania walio wengi kumpa ridhaa ya kuwaongoza.
Macho na masikio ya Watanzania yataelekezwa Dodoma, ambako ndiko uzinduzi huo unafanyika, ambapo pia wabunge wapya na wa zamani watapata fursa ya kukutana na kufahamiana zaidi.
Kama ilivyo miaka yote, Bunge la safari hii pia litakuwa na idadi kubwa ya wabunge wa CCM, ambao kwa vyovyote watakuwa na mtihani wa kupambana kwa hoja na wenzao wa vyama vya upinzani vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo.
Wakati maandalizi ya kikao hicho cha uzinduzi yakiendelea, mchakato wa kumpata Spika na Naibu Spika nao unaendelea ili siku ya siku ikifika viongozi hao wa Bunge wawe wamechaguliwa.
Tayari CCM imeshampitisha mbunge wa Kongwa, Job Ndugai kuwa mgombea wake wa nafasi ya Uspika. Katika bunge lililopita, Ndugai alikuwa Naibu Spika.
Kamati ya wabunge wa CCM iliamua kumpitisha Ndugai kuwa mgombea wa nafasi hiyo, baada ya wagombea wengine wawili, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulla Mwinyi na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson kuamua kujitoa.
Taratibu hizo zinafanywa huku tayari aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa ametoa tamko lake kuhusu uchaguzi mkuu.
Akizungumza na wanahabari juzi, Lowassa alisema matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), yakimpa ushindi aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli si halali. Lowassa akasema alichopoteza ni pambano, lakini hajashindwa vita.
Tofauti na alivyopata kusema huko nyuma baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kwamba akishindwa atarejea kijijini Monduli kuchunga mifugo yake, safari hii amesema atajikita zaidi katika kuendeleza mapambano ya kisiasa.
Alisema chini ya Katiba ya sasa ya nchi, ni dhahiri uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki na hivyo atapambana ili kupatikana Katiba mpya, ambayo itatoa mwongozo mzuri utakaowezesha kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.
Ikumbukwe kuwa yeye ni miongoni mwa waliokataa Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba, lakini sasa baada ya kushindwa urais, anaiona ni njema na anaitetea ili iandikwe kwa mwelekeo ambao awali aliukataa.
Katika msimamo wake mwingine kutokana na kutotambua matokeo yaliyotangazwa na NEC na kwa kuwa Katiba hairuhusu matokeo hayo kupingwa mahakamani, yeye na Ukawa hawautambui urais wa Dk Magufuli.
Msimamo wa Lowassa unashajiishwa na wa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye amekaririwa akisema watapinga hata hotuba ya Dk Magufuli ya uzinduzi wa Bunge la 11 na safari hii si kwa kutoka nje, bali kwa kusimama wakati wote akihutubia ili kupinga yaliyomo katika hotuba hiyo na nafasi yake ya urais.
Katika hotuba zake zote za kampeni na hata ya kutoa shukurani siku anaapishwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Novemba 5, mwaka huu, Rais Magufuli alisema hatabagua Watanzania kwa itikadi zao na kuwataka wanasiasa kukubali matokeo na kuungana naye kuwasaidia wananchi.
Mara zote Rais Magufuli alisisitiza kuwa yeye ni Rais wa wote na si wa CCM tu kwa kuamini kwamba, jukumu alilonalo ni la kuwasaidia Watanzania bila kujali waliompigia au waliomnyima kura, kwa kuwa wote wana haki ya kuishi katika nchi hii na kuhudumiwa kwa usawa.
Kwa kuwa Rais aliwasihi Watanzania kuwa wamoja na kuacha kubaguana, lingekuwa jambo jema kama wangemwelewa na kukubali hisia zake za moyoni na kumpa miaka yake mitano athibitishe kauli zake na si kumwekea vikwazo ambavyo vitamnyong’onyeza.
Wapinzani hususan wa Ukawa, wanapaswa kuelewa kuwa mwisho wa uchaguzi ni mwanzo wa uchaguzi mwingine, na kwamba miaka mitano si mingi, hivyo kusubiri hadi 2020 si tatizo na wavute subira wakati huo ukifika waingie ulingoni kujaribu bahati nyingine.
Kitendo cha kuingia bungeni na kusimama wakati wote ambao Rais atakuwa anahutubia, kwanza ni kinyume na kanuni za Bunge, lakini pia ni kumkosea adabu mtu ambaye amechaguliwa na Watanzania asilimia 54 ya waliopiga kura.
Kumfanyia dhihaka na dharau Rais ni sawa na kuwafanyia dhihaka na dharau Watanzania wote waliomchagua, ni vema basi wakamsikiliza Rais na kumpa fursa ya kuzindua Bunge kwa utulivu  na hasa ikizingatiwa kuwa wabunge wa Ukawa nao watakuwa ndani.
Mimi sidhani kuwa kusimama bungeni kuonyesha kumpinga Rais na serikali yake ni jambo lenye siha kwa mustakabali wa Taifa, bali ni kutaka kuonyesha jeuri ambayo haitazaa matunda yoyote.
Mwaka 2010, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Wilbrod Slaa, alikuja na msimamo kama huo. Baadhi ya wabunge wa upinzani nao kwa pamoja wakaamua kutoka nje na kuwaacha wa CCM, UDP na TLP, wakimsikiliza Rais Jakaya Kikwete akizindua Bunge hadi mwisho.
Hata hivyo, waliotoka nje walirejea siku nyingine na kuendelea na Bunge kama kawaida na hatimaye Rais Kikwete aliendelea kuongoza Taifa kwa miaka mingine mitano ya awamu ya pili na kumaliza salama Novemba 5, mwaka huu.
Kwa kurejea hilo, ni matumaini ya Watanzania  wengi kuwa wapinzani safari hii wataiona mantiki na kukubali kumsikiliza Rais Magufuli wakiwa wamekaa na kutafakari ujumbe atakapokuwa anawasilisha, badala ya kukaidi kanuni za Bunge eti kwa sababu hawatambui ushindi wake.
Watanzania wasio wabunge wana hamu ya kumsikiliza Rais wao mpya na kujua anawaahidi kitu gani katika kukabiliana na matatizo na kero walizonazo. Bila shaka hawana haja ya kushuhudia malumbano kati yake na wabunge wasioamini wala kukubali ushindi wake.
Ni bora hata wakaacha kuingia bungeni ili walio tayari kumsikiliza wamsikilize, lakini kama watang’ang’ania walichopanga kufanya, basi bila shaka Katibu wa Bunge na uongozi mzima wa Bunge wataona nini cha kufanya ikiwa ni pamoja na kuangalia suala la posho zao.

No comments:

Post a Comment