NA MWANDISHI WETU
WAKATI wananchi wa Zanzibar wakisubiri kwa hamu
kutangazwa kwa tarehe ya marudio ya uchaguzi, hujuma mbalimbali zimeanza
kufanywa ili kuhakikisha uchaguzi huo unavurugika.
Baadhi ya wanasiasa wakiwemo wafanyabiashara wakubwa,
wamekuwa wakishiriki kuandaa na kutekeleza hujuma hizo kwa maslahi binafsi na
uchu wa madaraka.
Habari za kuaminika zinasema kuwa, miongoni mwa
hujuma hizo ni pamoja na ile ya kuvishawishi baadhi ya vyama kususia uchaguzi
huo, wakilenga kuiaminisha jumuia ya kimataifa kuwa hali si shwari.
Mikakati ya hujuma hizo imedaiwa kusukwa na wanasiasa
(majina na vyama vyao yanahifadhiwa), ambapo tayari baadhi ya viongozi wa vyama
kadhaa wamewezeshwa kifedha ili kukubaliana na mpango huo haramu.
“Wapo watu wachache wanapenda kuona Zanzibar ikiwa
kwenye mgogoro kwa maslahi yao binafsi, ikiwemo kuendelea kusikika kisiasa
licha ya kuwa wamechoka. Hivi sasa wanaendelea na utekelezaji wa hujuma
kuhakikisha uchaguzi unakwama kwa kuvishawishi baadhi ya vyama kususia
uchaguzi.
“Kuna taarifa za uhakika kuwa baadhi ya viongozi wa
vyama wamepewa mgawo ili kufanikisha mpango huo haramu.
“Lakini kamwe hawatafanikiwa kwa sababu wananchi wako
pamoja na wanajiandaa kushiriki uchaguzi wa marudio kwa amani na utulivu,”
kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kimesema lengo la mtandao huo ni
kuhakikisha kunazuka vurugu pindi tarehe ya uchaguzi itakapotangazwa na
kuaminisha umma kuwa mgombea wa chama kimoja cha upinzani, anaungwa mkono.
“Kuna chama kinataka kionekana kinaungwa mkono na
vyama vingi vya kisiasa nchini ili vurugu zikianza, kipate huruma na kutetewa
na jumuia za kimataifa,” kiliongeza chanzo chetu.
Hata hivyo, kutokana na mikakati ya hujuma hizo,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk. Ali Mohammed Shein, imewahakikishia
wananchi kuwa suala la amani na utulivu halina mjadala.
Pia, imesema imejipanga kikamilifu kuudhibiti mtandao
huo unaojipanga kuvuruga uchaguzi na kuwatoa hofu wananchi, wasisite kujitokeza
kushiriki uchaguzi pindi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itakapotangaza tarehe
rasmi.
Kutokana na kubainika kwa mkakati huo, Chama cha
Alliance for Democratic Change (ADC), kimeonya kuwa kamwe hakiko tayari kuhongwa
wala kususia marudio ya uchaguzi.
Badala yake ADC kimeitaka ZEC kuharakisha kutangaza
tarehe ya marudio ya uchaguzi ili kijiandae kushiriki na kitakuwa mstari wa
mbele kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupigakura.
Kimesema wananchi wanapenda haki, amani na utulivu na
kwamba, watatumia sanduku la kura kuwaweka viongozi madarakani na kamwe
hakiwezi kuwa sehemu ya kuvuruga amani.
Kimesema hakuna sehemu ya kupata haki ya matokeo ila
kupitia ZEC, hivyo wanaosusa ama wanaojipanga kususia kamwe hawajitambui.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ADC, Ayubu
Kimangale, alisema hakuna sehemu ya kupata haki ila ni ZEC, kwa kuwa ndio yenye
mamlaka ya matokeo kisheria.
“Sisi tunahimiza ZEC itangaze siku ya uchaguzi ili
tujiandae kikamilifu, vyama vinavyosusa havijitambui,” alisisitiza.
Alisema kama kuna vyama vimechukua pesa kususia
uchaguzi, ADC haitachukua pesa na kitashiriki uchaguzi ipasavyo.
Katika kujipanga kisiasa zaidi, chama hicho kimeteua
Kamati ya Uendeshaji Shughuli za Chama, itakayoongozwa na Jumapili Kaliki,
Makamu Mwenyekiti wake ni Khamisi Mohamed Kombo, Katibu wa kamati ni Zamila
Suleiman Mrisho na Naibu Katibu wa kamati hiyo ni Mvita Mangupili.
Wajumbe wa kamati ni Ibrahin Hassan Pogoro, Rose Swai
na Mtumwa Faiz Sadiki.
Kimangale alisema sababu ya bodi ya wadhamini ya
chama kuchukua mamlaka ya uendeshaji wa chama ni kutokana na Kamati ya Utendaji
ya Taifa, kushindwa kukipatia chama hicho ushindi katika uchaguzi mkuu
uliopita.
Alisema chama hicho kimebaini hujuma nyingi zilizofanywa
katika uchaguzi, ikiwemo kuhusika na uandikaji wa barua ya kutokuwa na mawakala
katika uchaguzi mkuu na kughushi sahihi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa bodi
ya wadhamini pamoja na kutunga takwimu za fedha ambazo hazikuidhinishwa na
kikao.
Alisema bodi hiyo ya wadhamini imewataka viongozi wote
wa kanda, mikoa, wilaya, kata, matawi na wanachama, kushirikiana na kamati
iliyoteuliwa katika kukiimarisha chama.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, alikiri kusikia mipango ya hujuma hizo,
ikiwemo baadhi ya vyama kuhongwa na kwamba mamlaka husika inazifanyia kazi
kikamilifu.
Alisema serikali inaamini kila chama kitashiriki katika
uchaguzi huo na imejipanga kuhakikisha unakuwa huru na haki kwa vyama vyote
hivyo, wananchi wasitishwe.
Aboud alisema serikali haipo tayari kuona amani na
utulivu vinatoweka kwa sababu ya uchaguzi.
Desemba 28, mwaka jana, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha
Salim Jecha, alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar, baada ya
kubainika kuwepo kwa dosari.
Dosari zilizobainika ni kwa mgombea urais kupitia
CUF, Seif Sharif Hamad, kujitangazia matokeo pamoja na idadi ya kura kuzidi
idadi ya wapiga kura.
No comments:
Post a Comment