Monday, 18 January 2016

MAOFISA WA POLISI WAINGIA MATATANI




NA MWANDISHI WETU, MWANZA 
WAKATI baadhi ya hoteli maarufu jijini Mwanza, zikitajwa kuwa kituo cha kupanga mikakati ya ujambazi, biashara haramu ya dawa za kulevya na pembe za ndovu, baadhi ya vigogo ndani ya Jeshi la Polisi mkoani hapa, wanadaiwa kuhusika kwenye mtandao.
Mbali na biashara haramu, maofisa hao na baadhi ya wakaguzi, wakiwemo waliokaa kwa muda mrefu jijini hapa, wanatajwa kuendesha kantini ya jeshi hilo iliyoko Mabatini na baa za vinywaji za jeshi hilo za Mabatini na Nyakato, kama mirija ya ulaji. 
Uchunguzi uliofanywa na Uhuru, umebaini baadhi ya vigogo wa jeshi hilo wakiwemo waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali, wana hisa ama wanamiliki hoteli hizo kwa migongo ya watu wengine. 
Kutokana na kumiliki hoteli hizo, wamekuwa wakikutania katika vitega uchumi hivyo pamoja na maajenti wa biashara hizo haramu, kupanga mikakati ya kuilinda na kuchukua migawo yao. 
Imedaiwa baada ya makubaliano na kupatiwa migawo au ahadi za fedha watakazopewa mara baada ya bishara hizo kufanyika, hutumia baadhi ya askari walio katika mtandao kuzilinda ama kusindikiza na ikitokea zikakamatwa, hutolewa amri ya kuachiwa mara moja. 
Uchunguzi huo umebaini kuwa baadhi ya maofisa hao, pia wamejengewa nyumba, kununuliwa magari na kuwekewa fedha katika akaunti zao huku wengine wakipewa hisa kwenye migodi (midogo na ya kati) ya kuchimba na viwanda vya kuchenjua dhahabu mkoani Geita na Mwanza, kama malipo ya kulinda.  
“Ni kweli hapa maofisa wengi wa polisi hupenda kukutania na wafanyabiashara mbalimbali hata hao unaosema wa biashara haramu, we ni mgeni ndiyo maana hujui kama mwenye hoteli hii na ile ya (alizitaja) zinamilikiwa na wakubwa wa polisi,” kilidai na kuhoji chanzo cha habari kilichoko katika hoteli moja wilayani Nyamagana. 
Kwa mujibu wa vyanzo vingine, vikiwemo vya ndani ya jeshi hilo, hoteli nyingine tatu zinazodaiwa kumilikiwa na maofisa wa polisi na kutumiwa kwa mikakati hiyo, ziko maeneo ya Pasiansi na Ghana, wilayani Ilemela. 
Aidha, vyanzo vyetu vya habari vimedai kuwa vigogo, ambao wamepata kuwepo jijini hapa na baadaye kuhamishwa, walitengeneza ama kuleta watu, ambao watakuwa tayari kulinda mali na maslahi yao huku wenyewe wakiendelea na majukumu mengine ya kikazi.
Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa, kantini ya polisi na baa zilizoko kwenye kambi ya mabatini na kituo cha Nyakato, ni miradi ya vigogo wa jeshi hilo, wakiwemo mameneja wake na wajumbe ambao baadhi wamekaa kati ya miaka 10 hadi 20 jijini Mwanza. 
Kutokana na kuwa na miradi ya ulaji, bei za bidhaa katika kantini hiyo ni sawa na zilizo katika maduka ya uraiani, jambo ambalo linaelezwa kutowasaidia askari wa chini, ambao kipato chao ni kidogo, tofauti na maofisa, licha ya kuwa kantini za jeshi hilo hazilipi kodi ya mapato. 
“Mfano bei ya kilo moja ya mchele hapa ni sh 2,000, vipande vitano vya sabuni ya kufulia sh. 1,200, lita tano za mafuta ya kula sh. 16,500, betri moja aina ya Panasonic sh. 800, sawa na uraiani, hili ni duka la polisi au la walanguzi kama raia,” kilihoji chanzo kimoja cha habari na kudai kantini hizo hazina ukaguzi. 
Bei zingine zinazo lalamikiwa kuumiza askari, ambazo hazitofautiani na zilizopo kwenye maduka ya uraiani ni unga wa sembe (kg 10 sh. 11,000/=), soda sh. 500 na pakti ya chumvi  sh. 1,000, huku bia pekee ndizo zikiuzwa kwa sh 1,400. 
Jitihada za kumpata Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Justus Kamgisha, jana, kuelezea tuhuma hizo, hazikufanikiwa kutokana na simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu bila majibu. Hata hivyo, jitihada zaidi ili kupata ufafanuzi wa kina zinaendelea.

No comments:

Post a Comment