NA KHADIJA MUSSA
SIMANZI, majonzi na vilio vimetawala nyumbani kwa aliyekuwa
Mkurungenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mhandisi, Suleiman
Suleiman aliyefariki dunia wakati akiogelea katika bahari ya hindi.
Suleiman alifariki dunia jana asubuhi akiwa njiani akipelekwa
katika hospitali ya Aga Khani mara baada
ya misuli kukaza ghafla alipokuwa akiogelea.
Akizungumza na Uhuru jana, Mwanasheria Mkuu na Ofisa Uhusiano
wa TAA, Ramadhan Maleta alisema marehemu huwa anautaratibu wa kufanya mazoezi
ya kuogelea kila siku asubuhi kutoka feri hadi Kigamboni.
Alisema jana asubuhi kama kawaida yake alikwenda Feri kwa
ajili ya kuogelea saa 12.00 ambapo aliogelea hadi Kigamboni na alipokuwa
anarudi alipata tatizo la kukaza kwa
misuli na kuishiwa nguvu.
Maleta alisema mwenzake aliyekuwa anaogelea nae alimuona na
kujaribu kumuokoa na kuomba msaada kutoka boti za wavuvi ambao walifika na
kumpeleka nchi kavu na kumpa huduma ya kwanza, ambapo alikuwa akiwa njiani
kupelekwa hospitali.
Alisema TAA imepata pigo kubwa kwa kupotea kiongozi mahiri
ambaye alikuwa hana majigambo wala hakuweka matabaka baina na wafanyakazi na
alishirikiana na wote bila kujali nyadhifa zao.
Alisema marehemu alikuwa miongoni mwa viongozi waanzilishi wa
kwanza wa TAA mwaka 1999 na atakumbukwa kwa mchango mkubwa alioutoa na
usimamizi wa ujenzi wa viwanja vya ndege vya Songwe na Mpanda.
Pia ujenzi wa awamu ya tatu ta Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julkias Nyerere (JNIA) na viwanja vingine vya ndege vinavyoendelea na ujenzi
katika mikoa mbalimbali nchini.
Baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo waliofika nyumbani kwa
marehemu walisikika wakilia huku wakisema kuwa TAA wameacha yatima na kwamba
pengo la Suleimani ni kubwa kwao na kwa taifa.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM, Abdallah
Bulembo alisema msiba huo umempa pigo
kuwa kwa kuwa ni rafiki mkubwa wa Suleimani tangu miaka 25 iliyopita.
Alisema Suleiman alikuwa mtu wa watu na hakuwa na makuu ambapo
mara ya mwisho kukutana na marehemu ilikuwa Alhamisi ya wiki iliyopita ambapo alikwenda osifini kwake.
Naye kaka wa marehemu, Farid Karamma alisema Suleima
atakumbukwa kwa ukarimu wake na alikuwa mtu wa kupenda watu na asiyependa
migogoro.
Alisema marehemu ameacha mke mmoja na watoto watatu wa kiume
ambao ni Mohammed, Said na Husam Suleima anayesoma katika shule ya sekondari
Mzizima Dar es Salaam.
Mwili wa marehemu uliwasili nyumbani kwake Upanda saa 7.25
mchana ukiwa katika gari la kubebea wagonjwa la msikiti wa Maamur ambapo saa
9.21 ulichukuliwa na kupelekwa msikitini hapo tena kwa ajili ya kuswaliwa, na
kisha kwenda kus\zikwa katika makabiri ya Kisutu
HISTORIA
Marehemu alizaliwa Mei 11 mwaka 1957 na kupata elimu ya msingi
katika shule ya Sokomhogo Zanzibar na
kisha kujiunga na shule ya sekondari ya Forodhani Dar es Salaam kuanzia mwaka
1972 hadi 1975.
Mwaka 1976 hadi 1977 alipata elimu ya kidato cha tano na sita
katika shule ya sekondari ya Azania na kisha kujiunga na chuo kikuu cha Mysore
nchini India kuanzia mwaka 1979 hadi 1984 alipohitimu shahada ya uhandisi
ujenzi.
Mwaka 1988 marehemu alisoma stashahada ya uhandisi wa viwanja
vua ndege katika chuo kikuu cha Civil Aviation Centre cha nchini Singapore.
Mwaka 2005 hadi 2007 marehemu alipata shahada ya uzamili
katika masuala ya biashara katika chuo cha Maastricht/ ESAMI-Arusha.
AJIRA
Marehemu aliajiriwa na serikali maka Mhandisi Msaidizi wa
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam kwa sasa JNIA mwaka 1984
wakati ikiwa chini ya iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Kutokana na uhodari wake katika marehemu alipanda vyeo mbalimbali hadi alipofdikia ngazi ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA kuanzia mwaka
2011 hadi alipofariki.
Katika kipindi cha uhai wake aliwahi kushika nyadhifa katika
bodi za taasisi mbalimbali kama
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya
Maji Dar es Salaam (DAWASCO), Mjumbe
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Pia alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC),
Mjumbe wa shirika la Posta Tanzania (TPC), Mjumbe wa Shirika la Rasirimali za
Reli (RAHCO) na mjumbe kampuni ya Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Kilimanjaro (KADCO).
No comments:
Post a Comment