Monday, 18 January 2016

MUTUNGI AWASHUKIAWANASIASA, VYAMA; ATAKA MGOGORO WA ZANZIBAR USIGEUZWE MTAJI WA KISIASA




NA RACHEL KYALA
MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ameviasa vyama na wanasiasa kutotumia mgogoro wa Zanzibar kusaka umaarufu wa kisiasa.
Pia, amevionya baadhi ya vyama vinavyojipanga kususia uchaguzi wa marudio visiwani humo kuwa, haviwezi kukwamisha kufanyika.
Hata hivyo, Jaji Mutungi ameiomba serikali kuiongezea nguvu ofisi yake ili kuiwezesha kuongeza uwezo wa kutatua migogoro pamoja na kutoa elimu kuhusiana na masuala yote ya kisiasa.
Kauli ya Jaji Mutungi imekuja ikiwa ni siku moja tangu UHURU kuibua mikakati ya baadhi ya vyama kuhujumu uchaguzi huo, ikiwemo kuhongwa fedha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, kuhusiana na mgogoro huo, Jaji Mutungi, alisema suala hilo linahitaji subira na hatua stahiki zinachukuliwa.
“Tayari tumeviambia vyama vya siasa visubiri mazungumzo ya viongozi yanayoendelea visiwani humo. Ofisi hii inavionya vyama na wanasiasa wanaojaribu kutumia mgogoro huo kama chachu ya kujiendeleza kisiasa,” alisema.
Aliongeza kuwa Baraza la Vyama vya Siasa, lipo mbioni kuingilia mgogoro huo, ambapo tayari limeshaandaa vikao kwa kuwa kwanza lilianza na ukusanyaji wa taarifa muhimu.
Jaji Mutungi, aliitaka jamii kuondoa dhana kuwa mgogoro wa Zanzibar ni wa kisiasa, bali ni wa serikali, kwa kuwa serikali ndiyo inayosimamia uchaguzi.
“Licha ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wapo pia viongozi wastaafu ambao ni wakongwe, wanaijua vizuri historia ya Zanzibar, hivyo tunawaamini na tunayo matumaini watasaidia,” alisema.
Alisisitiza kuwa wanaopaswa kupongezwa ni wananchi wa Zanzibar, kwa uvumilivu na kuonyesha ukomavu katika suala la kutunza amani katika kipindi hiki cha mgogoro na si kiongozi ama chama fulani.
“Tunawashukuru Watanzania kwani sasa wameiva katika suala la amani na tunawasihi wanasiasa kuacha kujaza siasa kwenye mzozo huo,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema vyama vya siasa vimekuwa vikihubiri kuhusu uzalendo, lakini uzalendo si maneno matupu bali ni moyo wa kuipenda nchi na watu wake.
“Licha ya kuonyesha nia ya kutotaka kususia bure bali pia kuhakikisha wanavuruga uchaguzi, lakini hilo litaiweka serikali katika nafasi nzuri ya kuimarisha usalama,” alisema.
Kuhusu lawama nyingi inazotupiwa ofisi hiyo juu ya masuala mbalimbali yanayojitokeza kuwa haiyashughulikii, aliutaka umma kufahamu kuwa haifanyikazi zake kwa kutumia vyombo vya habari, bali kuchukua hatua stahiki pindi jambo linapotokea.
Jaji Mutungi alitoa kauli hiyo kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa Baraza la Vijana wa Chadema wanataka kumpeleka Msajili wa Vyama vya Siasa mahakamani kuhusu bango lililoonekana Zanzibar kwenye sherehe za Mapinduzi, lenye maneno yenye itikadi za kibaguzi.
“Sheria inamruhusu yeyote kwenda mahakamani, waende, lakini inawapasa wajue nini wanafanya na si kukurupuka tu,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema zipo hatua ambazo wameshachukua kuhusiana na suala hilo na kwamba, hatua zaidi bado zinaendelea. Alisisitiza kuwa hawawezi kutoka kwa jamii na kuanza kueleza nini wanafanya.
Alitaka ofisi hiyo kuongezewa nguvu kisheria, ili kushughulika zaidi na uratibu wa shughuli mbalimbali za kisiasa, ikiwemo kutoa elimu kwa umma na kutatua migogoro.

No comments:

Post a Comment