UMOJA wa Wazazi wa CCM, umepitisha azimio la kwenda Zanzibar ili pamoja
na mambo mengine, kukikabili chama cha CUF ili kukizuia kwa mara nyingine tena
katika harakati zake za kutaka kutawala visiwani humo.
Uamuzi huo ni moja kati ya maazimio yaliyopitishwa na Baraza Kuu la
Taifa la Umoja huo juzi, Jumapili, katika kikao chake cha siku moja
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ulioko katika
Makao Makuu ya Chama, Barabara ya Nyerere mjini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kikao hicho
kumalizika, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM, Alhaji Abdallah Bulembo,
alisema katika kikao hicho cha kawaida, Baraza Kuu liliamua kupeleka timu
maalumu Unguja na Pemba, lakini hakutaja
majina ya viongozi wanaotarajiwa kupiga kambi katika visiwa hivyo.
Hata hivyo, Alhaji Bulembo aliweka angalizo kuwa timu hiyo ya viongozi
wa ngazi za juu ndani ya jumuia hiyo, watakwenda huko baada ya Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), kutangaza tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi mkuu wa Rais wa
Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.
Jumatano, Oktoba 28, mwaka jana, ikiwa ni siku tatu tu baada ya
kufanyika kwa uchaguzi mkuu uliopita, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kwa
niaba ya tume hiyo, alitangaza kufutwa kwa uchaguzi huo, hatua ambayo hata
hivyo imekuwa ikipingwa na wanachama na viongozi wa CUF, na pia wamekuwa
wakisisitiza kuwa hawatashiriki katika uchaguzi wa marudio pindi ukitangazwa
kufanyika.
Pamoja na Alhaji Bulembo kutotaja majina ya viongozi watakaokwenda
kupiga kambi Unguja na Pemba kwa ajili hiyo, uwezekano mkubwa ni kuwa timu hiyo
itaundwa na wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Taifa, baadhi ya wajumbe wa
Baraza Kuu na kuongozwa ama na yeye mwenyewe au Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo,
Mohammed Seif Othman.
Akizungumzia masuala mengine, alisema Baraza Kuu la Taifa katika kikao
chake hicho, lilifanya uteuzi wa mwisho wa wanachama 12 wa jumuia hiyo, ambao
wameomba kugombea nafasi nne zilizo wazi ndani ya chombo hicho.
Alisema sababu ya nafasi hizo kuwa wazi ni wajumbe wa Baraza Kuu la
Taifa waliokuwa wakiwakilisha mikoa ya Pwani, Njombe, Kagera na Kigoma, kuhamia
katika vyama vitatu vya upinzani vya CUF, Chadema na ACT– Wazalendo, mwaka
jana.
“Hivyo tumeteua wagombea watatu katika kila mkoa ili wakachuane kutafuta
mshindi atakayeingia katika Baraza Kuu (la Taifa) kwa ajili ya kujaza nafasi
hizo nne,” alisema Alhaji Bulembo, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,
kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho ya mwaka 1977, toleo la 2012 inayotumika
sasa.
Akizungumzia hatua nyingine, alisema jumuia hiyo inakusudia kujenga
jengo la kitegauchumi lenye urefu wa ghorofa 14, katika eneo la Mchikichini,
Ilala jijini Dar es Salaam, ambalo litagharimu sh. bilioni 13.5.
Aidha, Alhaji Bulembo aliwaambia waandishi hao wa habari kwamba, wakuu
wa shule tatu za sekondari za Mwembetogwa, iliyoko mjini Iringa, Tegeta na
Tabata za jijini Dar es Salaam, wamefikishwa mahakamani ili kujibu mashitaka ya
ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za ada kutoka kwa wanafunzi.
Sambamba na wakuu wa shule hizo, ambao hata hivyo hakutaka kuwataja
majina yao, wengine wanaoshitakiwa nao ni pamoja na wahasibu na maofisa
ununuzi.
Alisema
ubadhirifu huo umetokana na fedha za manunuzi ya mahitaji ya wanafunzi, ikiwemo
chakula, ambapo kwa kushirikiana na mkuu wa shule, maofisa ugavi na wahasibu
wametumia mwanya huo kuiba fedha hizo.
“Katika
hatua ya kuwafikisha mahakamani sio wakuu wa shule pekee ndo waliofikishwa
mahakamani, bali watu wote waliohusika katika wizi huo,”alisema.
Alizitaja
jumla ya fedha zilizopotea kuwa ni zaidi ya sh. bilioni mbili, ambapo katika shule
ya sekondari Tegata ni milioni 690, Tabata milioni 470 na Mwembetogwa ni sh.
milioni 920.
Alisema
wapo walimu wakuu wa shule mbili, wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani wakati
wowote kuanzia sasa huku akigoma kuwataja mapema ili wasije wakawatoroka.
“Lakini pia tunakusudia kuvunja bodi za shule zote zilizokithiri kwa
ubadhirifu wa fedha za shule zetu”, alisema na kuongeza kwamba, Baraza Kuu la
Taifa la Jumuia hiyo pia limewakemea na kuwaonya viongozi wake wanaojaribu
kuwakingia ‘kifua’ wahusika wa tuhuma hizo na kuwataka waache tabia hiyo mara
moja.
Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa Mkoa wa Mbeya, Fatuma
Kasenga, alitoa taarifa iliyoonekana kuukingia ‘kifua’ ubadhirifu huo wa
mamilioni ya fedha za shule zinazomilikiwa na jumuia hiyo mkoani kwake, hivyo
hatua ya Baraza Kuu la Taifa ya kutoa onyo hilo inaweza kuwa mwiba wa kisiasa
kwake na viongozi wenzake wa mkoa huo.
No comments:
Post a Comment