SERIKALI
imewasimamisha kazi wakurugenzi wawili kwa tuhuma za matumizi mabaya na
kuisababishia hasara ya zaidi ya sh. milioni 300.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene, amewataja wakurugenzi
hao kuwa ni wa Manispaa ya Kigoma, Mhandisi Boniface Nyambele na
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Suleiman Lukanga.
Taarifa
ilitolewa mjini hapa, jana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Rebecca Kwandu, alisema wakurugenzi hao
wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuridhia na kutekeleza maamuzi, ambayo
yameisababishia serikali hasara na upotevu wa fedha wa zaidi ya sh. milioni 300.
Alifafanua kuwa Mhandisi Nyambele, anakabiliwa na tuhuma ya uuzaji wa nyumba za halmashauri bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo na bila kibali cha waziri mwenye dhamana kama sheria inavyoelekeza.
Kwa upande wa Lukanga, anakabiliwa na tuhuma za ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa sh. milioni 92 na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Kakese sh. milioni 294.
“Kufuatia tuhuma hizo kwa wakurugenzi hao, Simbachawene amemteua Mkuu wa Idara ya Maji Mhandisi Sultan Ndilowa kukaimu nafasi ya Nyambele,” alisema.
Aidha, alisema waziri huyo amemteua Katibu Tawala Msaidizi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Lauteri Kaoni kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda badala ya Lukanga.
Kwandu
alisema, hatua inayofuata baada ya kusimamishwa kwa wakurugenzi hao ni serikali
kufanya uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo na watakapobainika kuhusika, mamlaka
husika itachukua hatua.
Kwa
mujibu wa Rebecca, Simbachawene amewataka wakurugenzi watendaji wa mamlaka za serikali
za mitaa kote nchini, kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria,
kanuni na taratibu zilizopo.
Alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote, ambao watakiuka matakwa ya sheria, kanuni na taratibu na kutoweka mbele maslahi ya umma.
Tayari
aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty,
amesimamishwa akituhumiwa kuhusika na ubadhirifu katika miradi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment