Thursday, 21 January 2016

MWACHENI JK APUMZIKE- KISENA





SAKATA la uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), limechukua sura mpya baada ya Mwenyekiti wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena, kuwataka washindani wake kibiashara wasitumie kampuni hiyo kama njia ya kumchafua Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, kuhusu kuhusishwa kwa familia ya Rais wa awamu ya nne, Kikwete, alisema kama kuna watu wanataka kumchonganisha na serikali au umma wa Watanzania, wafanye hivyo kwa kumlenga yeye na wasimhusishe Kikwete ama familia yake.
Alisema pamoja na kutolea ufafanuzi suala la kampuni yake kununua UDA, kumekuwa na kelele zisizokoma huku wanaofadhili tuhuma hizo wakitaka kuwachafua na watu wengine wasiohusika na kampuni hiyo.
“Wako watu bila haya wanasema Simon Group ilipata upendeleo kununua UDA, kwa kuwa mmoja wa wanahisa ni mtoto wa Kikwete. Huo ni uzushi wa kiwango cha juu, kampuni hii haijawahi kumilikiwa na watu kutoka nje ya familia ya Mzee Simon, ukiondoa Professa Kapuya (Juma) ambaye ana hisa asilimia tano tu,” alisema Kisena.
Aliwataka wabaya wake kama wanadhani ana makosa na anastahili kushambuliwa, waelekeze mashambulio hayo kwake na wasihusishe watu wengine wasiohusika.
Aliwataka wanasiasa wafanye siasa na wafanyabiashara wafanye biashara, badala ya kuendekeza fitna ambazo hazitaisaidia nchi.

No comments:

Post a Comment