Sunday, 10 January 2016

OPERESHENI WAHAMIAJI HARAMU YAANZA KWA KISHINDO, VILIO VYATAWALA, WACHINA WAANZISHA TIMBWILI

HATIMAYE operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wahamiaji haramu, wafanyakazi na wafanyabiashara wanaofanya shughuli ambazo watanzania wanaweza kuzifanya, imeanza rasmi.

Operesheni hiyo kwa upande wa Dar es Salaam, jana, iliibua vilio hasa kwa raia wa China, ambao walikataa kurudishwa makwao, huku wengine wakiingia mafichoni.

Katika hali ya kushangaza, baadhi ya Wachina waliokuwa wakifanya kazi na kuishi nchini kinyume cha sheria katika Kampuni ya CATIC International,  iliyoko mtaa wa Lugalo, kiwanja namba 22, walianziasha vurugu kubwa huku  wakikataa kurudishwa nchini kwao.

Wengine waliangua vilio vya haja na kuwapa wakati mgumu maofisa wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, waliokuwa wakiendesha operesheni hiyo.

Ilipofika saa sita mchana, maofisa uhamiaji, walivamia katika nyumba hiyo na kuomba hati za wageni  waliokuwa wakiwatilia shaka, ambapo wafanyakazi watatu wa kampuni hiyo walibainika kuishi nchini na kufanyakazi kinyume cha sheria.

Mmoja wao alijaribu kutoroka akijifanya anataka kwenda kuchukua hati zake, hali iliyowalazimisha maofisa uhamiaji hao kutoa muda  kwa uongozi wa kampuni hiyo kumsalimisha na kutoa onyo kwamba iwapo hawatafanya hivyo, watawajibishwa.

“Mmoja amekimbia, ninawaagiza nyie viongozi wake  ajisalimishe mara moja. Msipomleta wakati nyie ndiyo mlikuwa mnamhifadhi, mtawajibika,”alisema ofisa mmoja wa Idara ya Uhamiaji, ambaye alikuwa akisimamia  operesheni hiyo na hakutaka kutaja jina lake.

Baada ya muda mfupi raia huyo wa China alijisalimisha.

Hata hivyo, hali ya hewa ilibadilika ghafla katika eneo hilo baada ya mwanamke mmoja wa  kichina kugoma kuingia kwenye gari la idara hiyo  kwa madai kuwa hataki kurudi China.

Mwanamke huyo alisikika akipiga kelele kwa kutumia lugha ya Kiswahili huku akilia kwa sauti kubwa.

Jitihada za maofisa uhamiaji hao na Wachina wenzake kumshauri mwanamke huyo kuingia ndani ya gari,  hazikuweza kuzaa matunda, hivyo kulazimu kutumika nguvu za ziada.

Akionekana kujidhatiti kugomea  amri, mwanamke huyo alianzisha patashika, hali iliyozua taharuki katika eneo hilo huku ikizingatiwa kuwa Wachina ni maarufu kwa mchezo wa karate.

Mmoja wa  viongozi wa operesheni hiyo,  Nelson Kinabo, alisema hadi kufikia jana alasiri,  kamatakamata  ilikuwa ikiendelea.

“Tumewakamata wageni wengi  ila bado hatuna idadi kamili. Tukikusanya nitakwambia maana ndiyo tunaendelea kukusanya idadi hiyo kutoka vikosi vyetu vilivyoko sehemu mbalimbali za jiji,”alisema  Kinabo.

Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Mkoa wa Dar es Salaam, John Masumule, alisema jana kuwa, operesheni hiyo inafanyika mkoa mzima wa Dar es Salaam na itahusisha nyumba hadi nyumba, ofisi hadi ofisi na mtaa kwa mtaa.

“Operesheni imeanzia Kariakoo na inaendelea mkoani kote. Kikubwa tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa maofisa wetu kuwafichua wageni wanaowatilia shaka kuishi nchini kinyume cha sheria,”alisema  Masumule.

Juzi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni,  alisema operesheni hiyo inalenga kuwakamata, kuwafikisha mahakamani na kuwarejesha makwao wageni hao wanaoishi, kufanyakazi na biashara  kinyume cha sheria  au kufanya shughuli ambazo Watanzania wanaziweza.

No comments:

Post a Comment