TANGU serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, ilipoingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, imefanya mambo mengi makubwa ikiwa ni pamoja na kuokoa zaidi ya sh. trilioni moja, zilizokuwa zitumike kwa matumizi yasiyo ya lazima.
Mambo mengine mazito, ambayo yamefanywa na serikali hiyo, ambayo jana ilitimiza siku 60, ni pamoja na kupiga marufuku safari zote za nje kwa watumishi wa serikali, ambazo sasa zitaruhusiwa kwa kibali maalumu.
Aidha, Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake, Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti walitembelea maeneo mbalimbali muhimu kwa uchumi wa nchi, zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA) na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kubaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali kabla ya kuchukua hatua.
Rais Magufuli pia alitangaza kufutwa kwa maadhimisho ya Siku ya Uhuru, yaliyopangwa kufanyika Desemba 9, mwaka jana, na kuagiza sh. bilioni nne, ambazo zingetumika, zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Morocco kwenda Mwenge. Kazi hiyo imeanza.
Mbali na hilo, Rais Magufuli, kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitangaza kufutwa kwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani na akaelekeza kwamba fedha zilizopangwa kwa ajili ya sherehe hizo zitumike kununua dawa za kufubaza makali ya ukimwi (ARVs).
Rais Magufuli pia aliagiza sh. milioni 225 zilizokusanywa kwa ajili ya hafla ya wabunge, iliyokuwa ifanyike mjini Dodoma, zitumike kununua vitanda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Tayari fedha hizo zimeshatumika kununua vitanda 300, magodoro 300, mablanketi na viti 30 vya magurudumu.
Utendaji huo wa serikali ya Rais Magufuli ndani ya siku 60, umeelezewa kuwa ni wa mfano wa kuigwa na viongozi wa Afrika na umekuwa ukisifiwa ndani na nje ya nchi huku ukidhihirisha wazi kauli mbiu yake ya 'Hapa Kazi Tu'.
Kinachofurahisha zaidi ni kuona kuwa, hata mawaziri aliowateua kushika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali, wameshaanza kuchukua hatua zinazofanana na zile zilizochukuliwa na Rais Magufuli na hivyo kwenda sawa na kasi anayoitaka.
Kwa mfano, mapema wiki hii Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, aliwatimua wakurugenzi wote wa Bodi ya NARCO, yenye dhamana ya kusimamia Ranchi za Taifa, kutokana na kushindwa kukamilika ujenzi wa Ranchi ya Taifa ya Ruvu.
Mwigulu, alitangaza uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya siku moja kwenye ranchi hiyo ili kukagua ujenzi wa majengo ya machinjio ya kisasa, ulioanza mwaka 2010, ambapo alibaini kuwepo na ubadhirifu wa sh. bilioni 5.7.
Aidha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, naye alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohamed Kikondo na watendaji wengine wa wizara hiyo kwa kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato, unaotokana na rasilimali za misitu na kuiingiza serikali hasara.
Profesa Maghembe pia amewasimamisha maofisa wa misitu wa mikoa nchi nzima ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya serikali, baada ya kubaini ubadhilifu unaofanywa na maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika mikoa na wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko mkuu wa serikali.
Hizi ni baadhi tu ya hatua ambazo zimeshaanza kuchukuliwa na serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli, kupitia kwa mawaziri wake, ambao wameonyesha dhahiri kupania kukifanya kile wanachotakiwa kwa lengo la kurejesha imani kwa wananchi na kuifanya Tanzania iwe nchi ya neema.
Katika hotuba yake aliyoitoa wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma, Rais Magufuli aliahidi kupambana na mafisadi, kubana matumizi, kuhimiza utendaji kazi, kuinua uchumi na kulinda amani na utulivu. Ni dhahiri kuwa hayo yote ameshaanza kuyatekeleza na mengi zaidi yatafanyika katika siku chache zijazo.
Tunampongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi uliotukuka huku tukiwataka Watanzania kumuunga mkono na kumpa nguvu zaidi ili aweze kuendelea kuitumikia nchi yetu kwa faida ya wananchi na pia kuwakomboa kiuchumi.
Vilevile tunawapongeza mawaziri ambao wameonyesha mfano kwa kuwachukulia hatua watendaji wabovu na wale waliobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma katika sehemu zao za kazi. Ni vyema mawaziri hao na wengine wakaze buti na kuendelea kuchukua hatua zaidi dhidi ya watumishi wenye tabia ya kutumia fedha za serikali kujineemesha.
Tunatoa mwito kwa wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano katika utendaji wake wa kazi ili iweze kuchukua hatua zaidi katika kupambana na rushwa, ufisadi na kuinua uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment