Thursday, 7 January 2016

TRA YAVUKA LENGO LA UKUSANYAJI MAPATO


MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA), imesema imevuka lengo la makusanyo ya kodi kwa Desemba, mwaka jana, ambapo imekusanya sh. trioni 1.4 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Imesema makusanyo hayo ni ongezeko la wastani wa sh. bilioni 490, kwa mwezi, ikilinganishwa na miezi ya Julai hadi Novemba, ambapo ilikusanya sh.bilioni 900.

Katika hatua nyingine, TRA imekusanya sh.bilioni 11, kutoka kwa wafanyabiashara walioandikisha makasha kutoka katika bandari kavu kinyume na taratibu za forodha.

Makusanyo hayo yanajumuisha sh.bilioni 5,383,945,204.61, kutoka kwa kampuni na wafanyabiashara 19, ambao wamemaliza kulipia kodi ya makasha, huku kampuni na wafanyabiashara wengine, ambao wamelipa sehemu ya kodi ya makasha na sh.bilioni 4,172,237,230, kutoka kwa mmiliki wa bandari kavu Azam ICD.

Akizungumza jana, Dar es Saalam, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata,  alisema hata hivyo wafanyabiashara watano bado hawajalipa kodi ya makasha ya sh. bilioni 2,005,923,687.76 na kwamba hatua za kisheria zinaendelea dhidi yao baada ya kuisha muda wa msamaha wa Rais, Dk. John Magufuli.

Kidata alisema katika kipindi cha Julai hadi Desemba, TRA ilikusanya sh. trilion 6,449,351, ikilinganishwa na lengo lilokuwepo la sh. trioni 6,597,710, ambayo ni sawa na asilimia 95 ya makusanyo yote.

“Kuongezeka kwa makusanyo ya kodi katika kipindi hiki kunatokana na mikakati madhubuti ambayo TRA imeiweka tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani na kuitekeleza, ikiwemo kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuweka mifumo mizuri ya ufuatiliaji na kumrahisishia mlipa kodi kulipa kodi anayostahili bila usumbufu na kwa haraka,” alisema.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu, TRA imepanga mikakati ya ukusanyaji mapato kwa kufuatilia kwa karibu vyanzo vyote vya mapato ili kuziba mianya yote iliyokuwepo.

Alisema TRA itaendelea kuwabana watumishi wasio waaminifu na kuwachukulia hatua mara moja ili kuwarahisishia wafanyabiashara
kulipa kodi.

“TRA itaendelea kuboresha huduma zake kwa kuondoa vikwazo kwa njia ya uwazi na haki, kushirikiana na wananchi katika kutoa taarifa za viashiria vya ukwepaji wa kodi na kuimarisha udhibiti wa bandari bubu zinazotumika kuingiza bidhaa za magendo,”alisema kamishna huyo.

Kidata alisema kwa sasa jitihada zinaendelea kuhakikisha wanafuatilia misamaha inayotolewa kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kulipa ushuru na kodi stahiki.

No comments:

Post a Comment