WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa
Makame Mbarawa, amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
imeanza kufanya uchunguzi ili kubaini ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya
watendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA).
Profesa Mbarawa alisema hayo jana, Dar es Salaam,
alipokuwa alitoa mwelekeo wa utendaji wa shirika hilo kwa watendaji na
watumishi wa TAZARA.
Alisema serikali ya awamu ya tano inalitaka shirika hilo
kufanya kazi kibiashara kwa kuhudumia wasafiri na wasafirishaji kikamilifu ili
kuinua uchumi wa shirika hilo na kuliondolea unyonge na migogoro ya mara kwa
mara.
Kuhusu ubadhirifu unaotokea TAZARA, Profesa Mbarawa
alisema tayari uchunguzi unaofanywa na TAKUKURU umeanza na kwamba hatua za
kisheria zitachukuliwa kwa wahalifu wote bila kujali wanatoka upande gani wa
TAZARA.
Aliwataka watendaji na wafanyakazi wa shirika hilo
kufanyakazi kwa umoja, uwazi na uadilifu ili kufikia malengo yaliokusudiwa na
kuhuisha ustawi wa shirika.
“Acheni
kufanyakazi kwa upendeleo na usiri kwani huo ndio mwanzo wa hujuma na
ubadhirifu, hali inayochochea malalamiko na kudumaza TAZARA,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa TAZARA, Betram
Kiswaga, alisema shirika hilo linakabiliwa na changamoto za kimtaji, kiufundi
na upungufu wa injini na mabehewa, hivyo ameiomba serikali kuiwezesha ili imudu
kujiendesha.
Alisema tayari shirika hilo limeanza kupata
wasafirishaji wa uhakika, hivyo kuimarika kimtaji kutavutia wasafirishaji wengi
zaidi.
No comments:
Post a Comment