WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
amewataka watendaji wa wizara na wakuu
wa taasisi zilizo chini yake, kukubali kubadilika kwa kufanyakazi kwa bidii.
Amesema watendaji hao wanapaswa kuhakikisha kuwa
sekta za nishati na madini zinakuwa na
manufaa makubwa kwa taifa, ikiwemo mabadiliko kiuchumi.
Profesa Muhongo aliyasema hayo juzi, mjini Dar es
Salaam, wakati wa kikao cha utambulisho wa viongozi wapya wa wizara.
Kikao hicho kilihusisha menejimenti ya wizara, taasisi
zilizo chini yake, zikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la
Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC), Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA),
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo
cha Madini Dodoma (MRI) na watendaji kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa
(NDC).
“Ni lazima tujitume. Hili ndilo jukumu letu la
kwanza. Wananchi wanataka umeme na wanataka mabadiliko kupitia sekta za nishati
na madini.
“Pia tunatakiwa tufanyekazi kwa umoja na uwazi kwa
sababu tumepewa fursa ya kuwatumikia wananchi hivyo ni lazima tubadilike na mabadiliko
ni lazima. Asiyeweza kuendana na kasi ya awamu hii aondoke, hakuna
atakayeonewa,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Aliongeza kuwa kutokana na uzoefu wa viongozi hao
na watendaji wa wizara na taasisi, anaamini yatakuwepo mabadiliko makubwa katika
sekta hizo kutokana na sifa zao kitaaluma na kiutendaji.
“Wananchi wana imani kubwa na uteuzi wetu na uwepo
wetu katika
wizara. Tufanyekazi kwa manufaa ya taifa letu,” aliagiza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo,
Profesa Justin Ntalikwa, alisema uongozi huo mpya unatarajiwa kufanyakazi kwa
uadilifu na umakini mkubwa.
“Jukumu lililo mbele yetu ni kubwa. Tunahitajika
kufanya kazi kwa bidii, tukitumia uzoefu wetu katika kutekeleza majukumu yaliyo
mbele yetu,” alisema Profesa Ntalikwa.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, anayeshughulikia masuala
ya madini, Profesa James Msofe, alisema anatarajia kujifunza kwa kasi kubwa
majukumu yake ili kuweza kufikia matarajio ya wananchi na taifa.
No comments:
Post a Comment