CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, kimesema utumbuaji majibu unaofanywa na Rais Dk. John Magufuli kwenye serikali, kwa sasa unapaswa kuhamia ndani ya Chama.
Kimesema lengo liwe ni kuondoa kasumba ya baadhi ya viongozi wa CCM kujiona bora zaidi na kutumia vibaya madaraka yao na kufanya ubadhirifu katika miradi ya Chama na jumuia zake.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Dk.Walid Kabourou, alisema hayo jana, wakati akifungua kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Jumuia ya Wazazi mkoani hapa.
Dk. Kabourou alisema wapo baadhi ya viongozi kwa kutumia vibaya madaraka, wameuza mali za Chama kwa kujipatia maslahi binafsi au kujimilikisha mali za chama kinyume na utaratibu, hivyo kuwafanya wakose sifa za kuwa viongozi.
“Rais Magufuli amefanya kazi kubwa serikalini ya kuwasafisha watendaji, ambao wanatumia vibaya madaraka yao, umefika wakati kile kinachofanyika kwenye serikali, kihamie kwenye Chama ili kuwasafisha watu wasiofuata utaratibu,”alisema.
Mwenyekiti huyo alisema ipo mifano hai ya majengo na viwanja, ambavyo ni mali ya Chama na jumuia zake, ambavyo viongozi wa CCM waliviuza na kujimilikisha isivyo halali.
Awali, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi mkoa Kigoma,Nicholous Zakharia, alisema pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitafanya tathmini ya uchaguzi mkuu na kuwachukulia hatua viongozi na wanachama waliokisaliti Chama wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita.
Zakharia alisema mbali na tathmini hiyo, pia wanaunga mkono hatua za utumbuaji majipu kwa viongozi wa serikali waliofanya ubadhirifu,matumizi mabaya ya madaraka na kuitia hasara serikali.
No comments:
Post a Comment