Saturday, 12 March 2016

MAWAKILI CHADEMA WAGONGA MWAMBA



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali mapingamizi ya awali yaliyokuwa yamewasilishwa na wanasheria wa CHADEMA, kupinga kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Mlimba, kupitia CCM, Godwin Kunambi.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Aloyisius Mujuluzi, baada ya kusikiliza hoja za pande zote husika katika shauri hilo kuhusu mapingamizi hayo ya awali.

Kunambi, ambaye ni mwanasheria wa CCM, alifungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo na mbunge, Suzan Kiwanga (CHADEMA).

Mwanasheria huyo wa CCM, alipinga matokeo ya uchaguzi huo kwa madai kuwa, uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na kwamba, uligubikwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi, hususan eneo la majumuisho ya kura kuanzia katika vituo.

Baada ya kufungua kesi hiyo, wanasheria wa CHADEMA, akiwemo Peter Kibatala, waliwasilisha mapingamizi ya awali yakupinga kesi hiyo, wakiomba mahakama kuifutilia mbali.

Jana, Jaji Mujuluzi alitoa uamuzi ambapo aliamua kutupilia mbali mapingamizi hayo kutokana na kukosa mashiko.

Jaji Mujuluzi alisema kesi ya msingi itasikilizwa mara tu baada ya mahakama kupanga tarehe ya kusikilizwa.

No comments:

Post a Comment