Saturday, 12 March 2016

MAKADA WATATU WATUMBULIWA MAJIPU KIGOMA



JUMUIA ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma, imewasimamisha viongozi wake waandamizi kwa tuhuma za kukisaliti Chama.

Mbali na kutoa adhabu hiyo, jumuia hiyo imetoa ushauri kwa vikao vya juu vya Chama, kuwafukuza uanachama viongozi hao.

Tamko hilo lilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Jumuia hiyo mkoani hapa, Nicholous Zakharia, ikiwa ni maazimio ya Baraza Kuu la Wazazi, katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika mjini hapa.


Zakharia aliwataja viongozi waliofukuzwa ndani ya jumuia hiyo kuwa ni mjumbe wa Baraza Kuu mkoa, Josephine Ntauheza, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake ya CCM wilaya ya Uvinza.

Wengine ni Gervas Nkagazwe, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Kibondo na mjumbe wa Baraza Kuu Wilaya ya Kibondo pamoja na Matoni Nyobeli, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Utekelezaji Wilaya ya Kibondo.

Alisema pamoja na baraza kuchukua hatua hiyo kwa viongozi hao, linaendelea kufanya tathmini na kuwachukulia hatua viongozi na wanachama wake, ambao watakwenda kinyume na Katiba ya chama na kanuni za uendeshaji wa jumuia hiyo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mwenyekiti huyo,
Katibu wa  jumuia hiyo mkoani hapa, Stanley Mkandawile, alisema maazimio ya baraza hilo yanaunga mkono mpango wa utumbuaji majipu, ulioasisiwa na Rais Dk. John Magufuli.

Awali, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma,Dk.Walid Kabouorou, aliitaka jumuia hiyo kuangalia na kuendeleza miradi  ya kiuchumi ili kuifanya isiwe ombaomba katika kuendesha shughuli zake.

No comments:

Post a Comment