Saturday, 12 March 2016
'WALIOISALITI CCM WASIONEWE SONI'
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Dodoma Mjini, mkoani Dodoma, wametakiwa kutowaonea haya na kuwafumbia macho wenzao waliokisaliti Chama wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Badala yake wametakiwa wawabainishe wazi katika vikao husika ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Akizungumza na mabalozi, wenyeviti na makatibu wa matawi wa CCM wa kata ya Dodoma Makulu, wakati wa mafunzo elekezi, Kaimu Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Salum Kali, alisema hakuna haja ya kuwaonea haya watu ambao hawakukitakia mema Chama.
Kali alisema tayari viongozi wa juu walishatoa agizo la kuwashughulikia wasaliti wote ndani ya Chama, hivyo kinachopaswa kufanyika ni utekelezaji katika ngazi zote bila aibu.
“Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ametoa kauli hiyo kwenye sherehe za kuzaliwa CCM pale Singida, na sisi wa chini ni lazima tutekeleze kwa kuwa wasaliti wametuumiza sana katika uchaguzi,"alisema.
Alisema walishindwa kujipanga vizuri kutokana na baadhi ya wanachama kuonekana nyakati za mchana wakiishabikia CCM, lakini usiku wanahamia kwenye vyama vingine vya siasa.
“Hao wasaliti ni lazima waondoke,hatuwezi kuwa na wanachama maslahi kwani wanakiua Chama chetu. Ni heri kubaki na jeshi dogo lenye mapenzi na Chama, kuliko kuwa na jeshi kubwa lisilokuwa na mapenzi na Chama,”alisisitiza Kali.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wanachama waliokihama Chama, Kali aliwataka viongozi wa kata na wanachama, kujipanga ili kuwachagua viongozi imara watakaokuwa mtaji wa uchaguzi mwingine unazokuja na watakaokuwa watekelezaji wazuri wa Ilani ya CCM.
Aliwaasa viongozi kuwa makini katika kupambana na changamoto zilizopo, kwani wakikosea hawatoweza kujenga misingi mizuri ya Chama, itakayoleta mageuzi ya kuichukua katika kata ya Njedengwa, iliyoko mikononi mwa upinzani.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo, Ephaim Kolimba, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kujua wajibu na majukumu yao katika utendaji kazi wa Chama na jumuia zake.
“Katika uchaguzi uliopita, tumeipoteza kata hii na viongozi hawa ukiwauliza wanasema hawakujua wajibu na majukumu yao, sasa tumeona tukae nao tunoane ili katika chaguzi zijazo tufanye kweli,"alisema Kolimba.
Alisema mafunzo hayo yataendelea katika kata nyingine na kuwasihi viongozi hao kwenda kuyafanyia kazi yote waliyojifunza, ikiwemo kuitisha vikao kwa mujibu wa katiba iliyopo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment