Saturday, 12 March 2016
SERIKALI YAAGIZA UCHAGUZI WA MEYA DAR UFANYIKE KABLA YA MACHI 25
SERIKALI imemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kuitisha kikao cha haraka cha uchaguzi wa meya na naibu meya, kabla ya Machi 25, mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI),George Simbachawene, amesema serikali ina dhamira ya dhati ya kutaka uchaguzi huo ufanyike haraka, kwa kufuata misingi ya kisheria na demokrasia ili wananchi wa jiji hilo waweze kupata huduma ya maendeleo kupitia viongozi watakaochaguliwa.
Kwa mujibu wa Simbachawe, kutokana na sintofahamu ya umeya wa jiji, jambo ambalo limechukua muda mrefu, anatoa wito kwa wadau wote wa vyama vya siasa pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kukaa kwa pamoja na kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika mapema iwezekanavyo
Alisema serikali haihusiki kwa njia yeyote ile katika sakata la kumpata meya wa jiji hilo na kwamba, wenye dhamana ya kujua kina nani, ambao ni wajumbe halali wanaotakiwa kushiriki uchaguzi huo ni vyama vya siasa husika pamoja na NEC.
Simbachawene alisema si kweli kama inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuwa, serikali ndio inayozuia
kufanyika kwa uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa Simbachawene, baada ya uchaguzi kuahirishwa mara kadhaa, ofisi yake ililazimika kuwasiliana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ili kujua ni kesi gani ya msingi imefunguliwa katika mahakama hiyo, ambayo inapinga uchaguzi huo kufanyika.
“Baada ya ofisi yangu kufuatilia kwa zaidi ya siku tatu, tulibaini kwamba kuna walalamikaji wawili, Suzan Masawe na Saad Khimji, waliofungua shauri namba 34/2016 dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, hali iliyosababisha uchaguzi huo kuahirishwa,”alisema.
Alisema hatua hiyo ilisababisha baadhi ya maofisa wa uchaguzi huo kupigwa na kuchaniwa nguo na baadhi ya madiwani, ambao walionekana kuwa na jazba, lakini kwa sasa anaamini uchaguzi huo utafanyika kwa haki na amani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment