Saturday, 12 March 2016

DK. LUMBANGA MKUU MPYA WA CHUO CHA ULINZI

RAIS Dk. John Magufuli, amemteua Balozi Dk. Matern Lumbanga kuwa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC), kwa kipindi cha miaka minne.

Uteuzi huo umeanza tangu Januari 15, 2016.

Chuo cha Ulinzi wa Taifa ni Taasisi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Chuo kilianzishwa Januari 4, 2012, kwa mujibu wa sheria za nchi na kupata Usajili na Ithibati kuanzi Mei 28, 2014.

Kozi zinazoendeshwa katika chuo hicho ni usalama na stratejia, ngazi za cheti, stashahada na shahada ya uzamili kwa watumishi wa serikali walio katika ngazi ya utungaji sera na kutoa uamuzi kwa maslahi na usalama wa nchi.

Baadhi ya washiriki wa kozi hizo ni maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Magereza, Usalama wa Taifa, Wizara na Taasisi nyingine za serikali.

Aidha, kuna washiriki kutoka nchi za SADC, Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi nyingine rafiki duniani hujumuishwa katika kozi hizo.

Balozi Dk. Lumbanga alizaliwa  Mei 5, 1947, katika kijiji cha Mchombe, wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.

Amehudhuria kozi mbalimbali za uhusiano wa kimataifa na ana shahada ya uzamivu katika uhusiano wa kimataifa, aliyoipata June 2009, katika Shule ya Kidiplomasia na Uhusiano wa kimataifa iliyoko Geneva, Uswisi.

Balozi Dk. Lumbanga ana uzoefu mkubwa wa kufanya kazi za kimataifa na katika Serikali ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Miongoni mwa madaraka makubwa aliyowahi kuyashika ni kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kati ya  2006 – 2012.

Pia, amewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais 1995 – 2006, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji 1992 – 1995, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara 1991-1992 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii 1987 – 1988.

No comments:

Post a Comment