Saturday, 12 March 2016

KUBENEA AUNGANISHWA KESI YA KUMJERUHI OFISA WA JIJI


MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea (CHADEMA), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuunganishwa katika kesi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Jiji la Dar es Salaam, Theresia Mbando, wakati wa uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Mbali na Kubenea, mshitakiwa mwingine aliyefikishwa mahakamani hapo jana na kuunganishwa katika kesi hiyo ni Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (CHADEMA).

Washitakiwa hao waliunganishwa katika kesi hiyo, ambayo inawakabili wabunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee, Mwita Waitara wa Ukonga, Diwani wa Kata ya Kimara, Ephrein Kinyafu na mfanyabiashara, Rafii Juma.

Kubenea na Njema walifikishwa mahakamani hapo mapema jana asubuhi na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, alidai mara ya mwisho washitakiwa wenzao walisomewa shitaka na waliomba hati ya kufika mahakamani kwa mshitakiwa Njema.

Alidai Njema yuko na ameongezeka mshitakiwa Kubenea, hivyo aliomba kuwasomea shitaka washitakiwa hao.

Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Mkeha, ambapo wakili huyo aliwasomea Kubenea na Njema, shitaka ambalo wanadaiwa kulitenda Februari 27, mwaka huu, katika ukumbi wa Karimjee, ulioko wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Ilidaiwa washitakiwa hao kwa pamoja walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha.

Washitakiwa hao walikana shitaka hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi unaendelea.

Hakimu Mkeha aliwaambia washitakiwa hao kwamba watajidhamini wenyewe kama walivyofanya wenzao kwa kutia saini dhamana ya sh. milioni mbili kila mmoja.

Kubenea na Njema walitimiza masharti hayo ya dhamana, hivyo kuachiwa kwa dhamana hadi Machi 16, mwaka huu, shauri hilo litakapokuja kwa kutajwa.

Kubenea alipandishwa kizimbani ikiwa ni siku moja baada ya kutiwa mbaroni akiwa mahakamani hapo kuhudhuria shauri linalomkabili la kumtolea lugha ya matusi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Juzi, Kubenea alikamatwa na askari akiwa mahakamani hapo na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kati na baadaye alirudishwa tena kusikiliza shauri hilo.

Baada ya shauri hilo kuahirishwam askari waliondoka tena na Kubenea kwenda kituoni kwa ajili ya kuhojiwa.

No comments:

Post a Comment