Friday, 1 July 2016

TRA KUFUNGUA OFISI RWANDA

Na Daudi Manongi, MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk Joseph Pombe Magufuli  amesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) watafungua ofisi nchini Rwanda ili kuraisisha  uhakiki wa bidhaa  kwa wafanyabiashara  wa  Rwanda wanaoingia nchini.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo Rais wa Rwanda Mhe.Paul Kagame anafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania ikiwemo ufunguzi wa Maonyesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Aidha amesema kuwa Serikali imetoa eneo la bandari kavu (ICD) kwa ajili ya kuhifadhia Bidhaa kutoka nchi ya Rwanda ili kupunguza urasimu ambao umekuwa kikwazo kwa maendeleo ya biashara hapa nchini na kwa namna hiyo biashara itakua kwani tunategemea uchumi utapanda kutoka asilimia 7 ya sasa mpaka asilimia 7.2.

Pia amesema kuwa Serikali imepunguza vituo vya ukaguzi barabarani kutoka Tanzania kwenda Rwanda kufikia vitatu na kwa kufanya hivyo itarahisisha safari za magari ya biashara njiani na hivyo kufikisha bidhaa kwa haraka.

Aidha amesema kuwa serikali iko mbioni kuanzisha kituo kimoja cha kukusanya mapato badala ya kila sehemu kuwa na mfumo wake ambao unapoteza mapato mengi kwa kuwa mifumo hiyo haina uthibiti mmoja na hivyo serikali ya Rwanda itasaidia kwa kuleta wataalamu wa Tehama ambao watasaidia kutoa mafunzo ili kusaidia mapato yetu kuwa katika udhibiti mmoja.

Kwa upande Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza Uchumi wa nchi izi mbili kwani zina historia ndefu na kwa kuendelea kufanya biashara pamoja nchi izi mbili zimejenga taswira mpya katika mahusiano.

Awali Mawaziri wa mambo ya Nje wa nchi za Tanzania na Rwanda walitia saini Muhtasari wa Tume ya Ushirikiano wa pamoja baina ya nchi hizi mbili.

No comments:

Post a Comment