Friday, 1 July 2016

NCHEMBA AWATANGAZIA VITA VIONGOZI, WANASIASA WACHOCHEZI


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema serikali imeweka utaratibu wa kuwashughulikia viongozi, wakiwemo wabunge na wanasiasa, ambao watakuwa wameanzisha na kuwaongoza Watanzania kufanya vitendo vya uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani.

Nchemba, alitoa kauli hiyo bungeni mjini hapa jana, wakati akiongezea majibu kwenye swali la nyongeza la Marwa Chacha (Serengeti-CHADEMA), lililoulizwa kwa niaba yake na Goodlucky Mlinga (Ulanga Mashariki-CCM).

Katika swali lake, Marwa alitaka kujua serikali inatoa kauli gani kuhusu vyama vya upinzani kuleta vurugu katika maeneo mbalimbali na kusababisha uvunjifu wa amani.

Pia, alitaka kujua serikali inasema nini kuhusu wabunge, ambao wamekuwa wakisababisha uchochezi kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, ikiwemo Jimbo la Ulanga Mashariki.

Nchemba aliwaonya wabunge na wanasiasa waliozoea maisha ya kupiga dili, kuacha tabia hiyo na kufuata sheria kanuni na taratibu za nchi ili waweze kuishi kwa amani na utulivu.

Alisema Watanzania wote wana haki sawa na ya daraja la juu, hivyo viongozi wanaowagawa kwa misingi ya kisiasa na kuwatengenezea chuki, wanapaswa kupuuzwa.

Aliwaasa Watanzania kutokubali kurubuniwa na kutengenezewa chuki na wanasiasa, ambayo baadaye inawasababishia kusambaratika.

Awali, akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema jeshi la polisi limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kanuni, hivyo halibagui mtu yeyote kwa vile linathamini Watanzania wote.

Naibu waziri alisema jeshi la polisi limekuwa likichukua hatua mbalimbali kwa viongozi wa vyama vya siasa, ambao wamekuwa wakisababisha vitendo vya uvunjifu wa amani na uchochezi.

Alisema kila mtu atashughulikiwa kulingana na kosa alilofanya bila kuangaliwa ana cheo gani.

“Iwe mbunge au kiongozi wa chama cha kisiasa, atachukulia hatua kulingana na matendo aliyoyafanya. Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inamlinda mbunge kwa kile anachokisema bungeni, lakini si kwa matendo ya uhalifu atakayofanya nje,”alisema.

Akiongezea majibu ya swali hilo, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harson Mwakyembe, alisema halikupaswa kuingia bungeni
kwani limekiuka masharti ya kanuni ya 40 ya kanuni za kudumu za Bunge.

Dk. Mwakyembe alisema kanuni zinataka kuletwa kwa maswali, ambayo yana ushahidi ili serikali iweze kuyajibu na si kuletwa kwa kubahatisha ndani ya bunge.

“Vifo vinavyozungumziwa kwenye swali hilo havijathibitishwa kitaalamu. Nawaonya viongozi hao wakiwemo wabunge, kutotumia siasa katika kuliendesha taifa kwani haliwezi kujengwa kwa mtindo huo,”alisema.

Baada ya Waziri Mwakyembe kutoa kauli hiyo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema swali lilipitiwa na Kitengo cha Sheria cha Bunge na kujiridhisha kwamba linastahili, hivyo wakati mwingine serikali nayo ijiridhishe kabla ya kuleta majibu bungeni.

Katika swali lingine la nyongeza, Kangi Lugola (Mwibara-CCM), alitaka kujua kauli ya serikali kwa Watanzania na wabunge, ambao wamekuwa na tabia ya kuhusisha kila kifo kinachotokea na masuala ya kisiasa, ambayo yanaweza kuleta uchochezi.

No comments:

Post a Comment