Tuesday, 13 December 2016

WAZIRI MKUU AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUWAHIMIZA WAUMINI KUJIEPUSHA NA CHUKI NA UCHOCHEZI




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao kwa kuwahimiza waumini wao kujiepusha na kauli na vitendo vitakavyopandikiza chuki na uchochezi miongoni mwa waumini  wa dini moja na waumini wa dini nyingine .

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu , Desemba 12, 2016) wakati akihutubia kwenye baraza la Maulid lililofanyika Shelui mkoani Singida, ambapo amesisitiza kwamba Serikali ya awamu ya tano ipo imara na haitayumba .

“Ni vyema tukatambua kwamba katika mifarakano na uhasama wa kidini hakuna atakayeibuka mshindi bali wote tutakuwa ni watu tulioshindwa . Nyumba za ibada zisaidie kuunganisha waumini na kuwa mfano usoni kwa jamii ,”

Amesema mara kadhaa watu wameshuhudia migogoro na mapigano kwenye Misikiti wakigombea uongozi na mali matukio ambayo hayana tija ndani ya Uislam, hivyo ni vyema wakafuata misingi ya dini ya kuheshimiana , kuelewana na kuvumiliana. Watumie mabaraza kukemea hali hiyo inayowagawa Waislam .

Amesema Serikali itaendelea kuzitegemea dini zote nchini  kujenga msingi imara wa kuleta amani miongoni mwa  Watanzania. Serikali itaendelea kusisitiza na kuheshimu uhuru wa raia wa Tanzania kuabudu dini wanayoiamini kwa sababu ni moja kati ya haki za msingi za kila mwananchi kwa mujibu wa  Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania

“Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kufanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba uhuru huo unaheshimiwa . Hii ni nyenzo muhimu iliyosaidia kulifanya Taifa letu kuwa ni mfano wa kuigwa kote ulimwenguni .Tutaendelea kushirikiana na viongozi wa dini zote nchini ili kuhakikisha kuwa tunu hiyo muhimu haichezewi na mtu au kikundi chochote,” amesema .

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alizungumzia suala la kuwepo kwa tishio la ugaidi duniani ambalo limegharimu maisha ya baadhi ya wananchi.” Aidha , mmezungumzia kuhusu uwezekano wa baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi kufunguliwa mashtaka kwa sababu ya chuki au kulipiza kisasi,”.

“Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali iko macho katika kupambana na tishio lolote la kiusalama ndani na lnje ya mipaka ya nchi yetu. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya utayari wakati wote ili kupambana na vikundi au watu na mtu yeyote mwenye nia ya kuhatarisha usalama wa nchi yetu,” amesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakukumbusha viongozi wa dini  kwamba jukumu la ulinzi wa nchi yetu kwa mujibu wa Katiba ni jukumu la kila mwananchi. “ Yaani kila Mtanzania,”.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa ni vyema viongozi wa dini wakatambua kwamba wao pamoja na waumini wanaowaongoza ndio walinzi wa Taifa hivyo wanalo jukumu la kuendelea kuwasihi waumini kuendelea kuwa raia wema na kutoa taarifa za dalili za uhalifu mapema iwezekanavyo .

“Mathalan , hawa watoto wanaojiita panya road huko Dar es Salaam au vijana wanaoteka magari pale mlima Sekenke , hawatoki kwenye sayari nyingine ni watoto wetu tunaishi nao majumbani , tunaabudu nao Misikitini au Makanisani. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuwaripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili watambulike na washughulikiwe ipasavyo. Wasiendelee kuleta madhara kwa raia wema ,” amesema .

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu  wa Tanzania Aboubakar Bin Zuber  amewasihi waislam nchini kuishi maisha ya Mtume Muhammad (SWA) ambaye alisisitiza kupendana na kushikamana ,kuwajali wengine bila kuwabagua kiimani ,kupenda kufanya kazi halali na kujifunza.

“Si jambo rahisi kupata kipato bila kufanya kazi ,tutalaumu kila siku kuwa hatuoni mabadiliko ya kipato wakati sisi wenyewe hatufanyi kazi. Uislam ni kielelezo tosha kwa mfano wa maisha bora, si kweli kuwa dini yetu inafundisha tuchukie wengine,” amesisitiza.

Pia Sheikh Zubeiry amewaasa waumini wa dini zote kushika imani iliyosahihi huku akiwaomba  kupuuza kauli za badhi ya watu kudai magaidi hutokea katika dini ya kiislam kutokana kuwa na imani kubwa ya kiislam.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba amesisitiza kupambana na watu ambao wamekuwa wakienda kinyume na sheria za nchi.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, DESEMBA 12, 2016.

No comments:

Post a Comment