Thursday, 18 May 2017
MTOTO ANAYEISHI KWA KULA SUKARI, MAFUTA YA KULA AFANYIWA VIPIMO
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imeanza kumfanyia vipimo mtoto Shukuru Kisango, anayedaiwa kuishi kwa kula sukari, maziwa na mafuta ya kula.
Mtoto huyo, ambaye picha zake zilienea kwenye mitandao ya kijamii, anadaiwa kuwa na hali mbaya kiafya, ikiwemo ngozi yake kusinyaa na kusikia maumivu makali pindi anapokosa vyakula hivyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MNH, Aminiel Aligaesha, alisema mtoto huyo aliwasili juzi, saa 12 za jioni kutoka wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Pia, alisema mtoto huyo amefika hospitalini hapo kutokana na agizo la serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto la kuwataka kumtafuta popote alipo kwa ajili ya matibabu.
“Tuliona picha kutoka kwenye mitandao ya kijamii ikimzungumzia mtoto huyo jinsi anavyopata maumivu na aina ya vyakula anavyokula. Baada ya hapo, tuliagizwa atafutwe popote alipo ili aletwe Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu," alisema.
Aligaesha alisema baada ya kufika hospitalini hapo, alipokelewa na kupelekwa idara ya magonjwa ya dharula na kufanyiwa uchunguzi wa awali kabla ya kulazwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Pia, alisema tayari mtoto huyo amefanyiwa vipimo vya damu, ambavyo vipo maabara kwa ajili ya kuchunguza zaidi kinachomsumbua.
“Kwa sasa madaktari wetu wanaendelea kumuangalia kwa ukaribu na madaktari wa fani zote watamfanyia vipimo vingine ili kubaini anachosumbuliwa kwa lengo la kujua mwenendo wa matibabu yake,” alisema.
Aligaesha alisema kwa kipindi chote atakachokuwepo hospitalini hapo, mtoto huyo hatachangia gharama yoyote ya matibabu.
Kwa upande wake, mama wa Shukuru, Mwanabibi Mtenje, aliishukuru serikali pamoja na uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa kumuhudumia mtoto huyo.
Alisema tatizo la Shukuru lilimuanza Aprili 10, 2001, ambapo alikuwa na dalili kama za homa na malaria hadi kufikia hapo alipo.
Alieleza kuwa, mtoto huyo anatumia mafuta lita moja, maziwa lita mbili na robo tatu ya sukari kwa siku, jambo ambalo lililowastua watu wengi.
“Hali hiyo ilikuwa inaniumiza kutokana na hali yangu. Mimi ni mjane na tatizo la mtoto na tiba, nilikuwa nashindwa kuzielewa,” alisema.
Alisema mtoto huyo akikosa vyakula hivyo, alikuwa anaumia mwili mzima kwani alikuwa akijihisi nyama zikiwa zinakatakata. Pia, alisema maumivu yakimuanza, mtoto huyo alikuwa hawezi kufanya kitu chochote.
“Ni mwaka wa 16 tangu Shukuru aanze kusumbuliwa na maradhi hayo, lakini ninashangaa tangu niwasili Muhimbili, sijaona akipata shida kama awali ila ninaamini atapona,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment