Monday, 29 May 2017
SERIKALI YATANGAZA KIAMA KWA MADALALI WA NYUMBA NA ARDHI
SERIKALI imesema kiama cha madalali wa ardhi na nyumba, kinakuja baada ya kutungwa sheria katika mwaka wa fedha 2017-2018.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017-2018.
Waziri Lukuvi alisema kuanzia sasa, serikali haitawafumbia macho matapeli, ambao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya maofisa wa wizara ya ardhi kunyanyasa wananchi.
Lukuvi alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia kisingizio cha mahakama kupora adhi za wananchi masikini na kujiuzia kwa njia ya udanganyifu.
Waziri huyo alisema serikali inaandaa sheria, ambayo itamlinda mmiliki wa nyumba au ardhi kukwepa kitanzi cha matapeli hao.
"Kiama cha matapeli wa nyumba na ardhi kinakuja, tuko mbioni kutunga sheria mwaka huu, ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi masikini. Matapeli wa ardhi na nyumba kuanzia leo (jana), wafunge maduka yao.
"Kumeibuka matapeli, ambao wanatumia mwanya wa mahakama kuwatapeli watu. Utakuta huku inatolewa Ijumaa, saa nane mchana kwamba, nyumba iuzwe na tapeli huyu anakuwa tayari kampanga mnunuzi, tena kwa bei ya kutupa. Kuanzia sasa hatutakubali," alisema Lukuvi.
Waziri huyo alisema matukio ya wananchi wasiokuwa na kipato kunyanyaswa, yapo katika maeneo mengi nchini na alitoa mfano mkoani Lindi.
Alisema baada ya kubaini madudu hayo, aliirejesha ardhi ya ekari 4,000, iliyoko katika eneo la 'beach' ya Lindi, kwa kujengwa zahanati.
Aidha, Lukuvi alisema wamiliki wa mashamba makubwa, ambayo hayakupimwa, wataanza kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Alisema baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo wanatumia mwanya wa maeneo yao kutokupimwa muda mrefu, hatua inayoikosesha mapato serikali.
Lukuvi alisema serikali inaandaa utaratibu, ambao utawalazimisha walimiliki wa ardhi zisizopimwa, kulipa kodi ya ardhi.
"Pale Dar es Salaam, kuna watu wanamiliki ardhi hekari 10,000 au 30,000 zote za nini? Halafu hawaziendelezi. Tunaandaa utaratibu, watakuwa wakilipa kodi kuanzia sasa," alisema Lukuvi.
Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi ametoa onyo kali kwa maofisa wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), walioshiriki kutoa hati za makazi 60,000.
Alisema maofisa hao wataingia matatani kwa kuwa rekodi zinaonyesha kuwa, hati zilizotolewa na CDA zilikuwa 60,000, lakini zinazomilikiwa ni 26,000.
Lukuvi alisema kuna harufu ya rushwa kwa watumishi wa mamlaka hiyo iliyovunjwa na Rais John Magufuli kwa kuwa hati 34,000, hazijulikani zilipo.
"Tutawasaka wote waliohusika na upotevu wa hati 36,000, ambazo hazijulikani zilipo, tutawakamata matapeli wote kwa kuwa wameingia sehemu mbaya, tunataka kujua ziko wapi," alionya Lukuvi.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeomba sh. 70,770,454, 748, kwa ajili ya matumizi mbalimbali katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Wakati huo huo, serikali imesema inatarajia kupunguza tozo ya mbele (premium) kutoka asilimia 7.5 hadi 2.5, ya thamani ya ardhi kuanzia Julai, mwaka huu.
Uamuzi huo wa serikali unatarajiwa kutoa fursa kwa wananchi wenye maeneo ya ardhi, kujitokeza kwa wingi kupimiwa na kumilikishwa ardhi.
Waziri Lukuvi alisema, hatua hiyo itakuwa na tija kwa wananchi kumiliki maeneo kwa gharama nafuu na kupanua wigo wa walipa kodi ya pango la ardhi.
Alisema ada hiyo itatozwa mara moja wakati wa umilikishaji ardhi kwa mujibu wa fungu la 31 la Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999.
Lukuvi alisema kupunguzwa kwa kiwango cha tozo ya mbele, kutavutia wananchi wengi kumilikishwa ardhi kwa mujibu wa sheria.
"Natoa rai kwa wananchi wote kutumia fursa hii ya punguzo la tozo ya mbele, kupima na kumilikishwa maeneo yao na kulipa kodi," alisema Lukuvi.
Alisema katika mwaka wa fedha 2017-2018, wizara hiyo inatarajia kukusanya sh. bilioni 112.5, kutokana na shughuli za sekta ya ardhi.
Waziri huyo alisema fedha hizo zinatarajiwa kupatikana kutokana na vyanzo mbalimbali vya kodi ya pango la ardhi, ada na tozo mbalimbali za ardhi.
Aidha, Lukuvi alisema katika kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi, wizara imeboresha muundo wa ofisi za kanda, kwa kuanzisha kanda mpya ya Simiyu, ili kupunguza na kuongeza mikoa katika baadhi ya kanda.
Aidha, Waziri Lukuvi amepiga marufuku baadhi ya taasisi binafsi kujihusisha na uaandaji wa ramani na kuziuza bila idhini ya wizara.
Alisema jambo hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria kwa kuwa baadhi ya ramani hazitoi tafsiri sahihi ya mipaka ya Tanzania na nchi jirani.
"Natoa rai kwa wote wanaojihusisha na shughuli hizo, waache mara moja, vinginevyo wizara haitasita kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani,"alionya Lukuvi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment