Na
Mwandishi Wetu
KWA takriban mwezi mmoja wa kampeni za uchaguzimMkuu,
mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ameanza kuonyesha namna urais wake
utakavyokuwa endapo Watanzania watampa nafasi hiyo.
Tayari watu wanaofuatana na Dk. Magufuli katika
kampeni hizo, wameanza kuona kwamba endapo atachaguliwa, Watanzania watakuwa
wamepata kiongozi mchapakazi, anayeheshimu kazi, anayejali muda na mwenye nia
ya kutatua kero za wananchi.
Dk. Magufuli (54), amejiwekea utaratibu wa kupata
kifungua kinywa mapema na baada ya hapo huchapa kazi hadi mwisho wa muda
unaoruhusiwa kisheria kufanya kampeni.
“Katika muda wote wa kampeni ambao tumekuwa na
Magufuli, tumemwona akila chakula cha mchana si zaidi ya mara tano. Yeye
akishakula asubuhi basi. Njiani atakunywa maji au kingine chochote, lakini
ndiyo hali tena hadi usiku.
“Kutokana na tabia yake hiyo, kuna watu sasa wameanza
tabia ya kujiwekea chakula na vinywaji kwenye magari kwa sababu wanajua
hawatapata muda wa kula mchana. Huyu bwana yeye ni kazi tu muda wote,” alisema
mmoja wa waandishi wa habari aliyemo kwenye msafara wa Magufuli tangu alipoanza
kampeni Agosti 23, mwaka huu.
Tabia hiyo ya Magufuli ndiyo imemwezesha kuwa mgombea
urais aliyekutana na wananchi wengi zaidi na kufika sehemu nyingi zaidi kuliko
wagombea wengine nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kwa kawaida, Dk. Magufuli hufanya mikutano mikubwa
mitatu kwa siku, lakini hufanya mingine midogomidogo kati ya mitano hadi nane;
inayofanyika mara nyingi katika maeneo ambako wananchi wamemsimamisha.
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya CCM, Abdallah
Bulembo, anayeongozana na mgombea huyo, alisema kazi ya kusaka kura ni ngumu,
lakini inakuwa ya kuvutia wakati Chama kinapokuwa na mchapakazi kama Dk.
Magufuli.
“Sikumbuki kama tumewahi kupitisha siku moja pasipo
kusimamishwa njiani na wananchi wanaotaka kumwona Dk. Magufuli na kumsikiliza.
“Anasimama kwa sababu anawapenda wananchi wake na hii
ni sifa kubwa kwa mtu yeyote anayetaka urais.
“ Mtu mwingine anaweza kuona kuwa ni mateso lakini
sisi tunaotaka ushindi wa CCM tunajisikia raha kuwa na Magufuli. Tulipomaliza
ziara yetu ya Morogoro na kwenda mkoa wa Tanga, tulisimamishwa njiani takribani
mara kumi na kote mgombea alisimama na kuzungumza. Kwa kweli mgombea wetu
anatupa moyo sana,” alisema Bulembo.
Kwa mujibu wa taarifa
rasmi ya CCM iliyotolewa wiki iliyopita, Magufuli alikuwa amefanya kampeni
katika mikoa 12 na majimbo 94. Pia, alikuwa amefanya mikutano mikubwa ya
hadhara 76 na mikutano ya barabarani 381.
Taarifa hiyo iliyotolewa na mmoja
wa wajumbe wa Kamati ya Kampeni ya Kitaifa ya CCM, January Makamba,
ilisema mgombea huyo ambaye ni Waziri wa
Ujenzi, aliyepata mafanikio makubwa katika ujenzi wa barabara za lami nchini,
amekwishatembea kwa gari jumla ya kilomita 13,720 na amekutana moja kwa moja na
asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura.
Gazeti hili limeelezwa pia kuhusu namna Magufuli alivyoweka msimamo wa
kutokutana na watu asiowafahamu au wenye historia tata wakati huu wa kampeni.
Kwa sababu ya ratiba ngumu ya kampeni, Magufuli amekuwa akifanya kazi
mchana na kujipa muda wa kusoma na kupumzika, na ameweka maelekezo ya
kutokutana na watu asiowajua.
“Wakati mwingine wagombea urais wanajiingiza kwenye matatizo bila ya
kufahamu. Magufuli hataki kukutana na watu hovyohovyo. Kama ni vikao rasmi
atafanya, lakini hana muda wa kupiga porojo na watu asiowajua au wanaoweza
kumharibia taswira yake na ya nchi kwa ujumla,” alisema mmoja wa wasaidizi wa
Magufuli aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina.
No comments:
Post a Comment