NA MOHAMMED ISSA, BUNGI- ZANZIBAR
MGOMBEA urais wa CCM Zanzibar, Dk.
Ali Mohammed Shein, amesema CCM ina uwezo mkubwa wa kuongoza nchi na kuwa hakuna
mbadala wa CCM.
Amesema CCM itaendelea kubaki kuwa
CCM na itaendelea kuongoza serikali kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi.
Dk. Shein alisema muundo wa serikali
ya umoja wa kitaifa, haukuja kwa lengo la kuleta vurugu na uvunjifu wa amani
bali ulikuja kuleta maridhiano na mshikamano kwa wananchi.
Alisema katika kipindi cha mwaka
mmoja na nusu uliopita, kumeibuka vikundi vyenye lengo la kuvuruga uvunjifu wa
amani na kuwagawa wananchi, hivyo
aliwataka wananchi wasikubali kugawanywa na watu wasioitakia mema Zanzibar.
Aliyasema hayo jana wakati
akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika uwanja wa mpira Bungi Wilaya
ya Kati Mkoa wa Kusini, Unguja na kuhudhuriwa na maelfu ya wana CCM na
wananchi.
“Tuna uwezo mkubwa wa kuongaza nchi,
hivyo hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi zaidi ya CCM,
ninawaomba muendelee kutuamini kwa kutupa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, mwaka huu,” alisema.
Alisema anaamini kuwa ataendelea
kuwa Rais wa Zanzibar, kutokana na mambo mengi aliyofanya visiwani humo.
Mgombea huyo akizungumzia Ilani ya
Uchaguzi ya CCM, alisema iliyopita imetekelezwa kwa asilimia kubwa na hivi sasa
Zanzibar, imepiga hatua ya maendeleo yakiwemo ya kiuchumi, kijamii na
miundombinu.
Alisema huduma za maji zimeongezeka
katika Mkoa wa Kusini Unguja na kufikia asilimia 76.6 ya upatikanaji wa huduma
hiyo ambapo Mkoa wa Mjini Magharibi umefikia zaidi ya asilimia 86.
Dk. Shein alisema katika miaka
mitano ya utawala wake, amefanikiwa kujenga mtandao wa barabara Unguja na Pemba
wenye zaidi ya kilomita 120, ambazo hivi sasa zinapitika kwa uhakika.
Kuhusu sekta ya kilimo alisema
kinachangia kwa asilimia 31 ya pato la taifa, hivyo serikali yake itaendelea
kuiboresha sekta hiyo.
Alisema mwaka jana na mwaka huu,
wamevuna tani zaidi ya 600,000 za kilimo
na mafanikio hayo yametokana na kuwepo kwa zana bora za kilimo.
Dk. Shein alisema nia ya serikali ni
kupunguza kuagiza mchele kutoka nje ya nchi na kwamba ifikapo mwaka 2018,
watafanikiwa kwa zaidi ya asilimia 60.
“Mafanikio yote haya yametokana na
juhudi kubwa ya serikali na juhudi zangu na za Chama changu hivyo asitokee mtu
yoyote akadai yametokana na yeye,” alisema.
Dk. Shein alisema sekta ya afya
imeimarishwa kwa kiasi kikubwa ambapo vituo vya afya vimeongezwa Unguja na
Pemba.
Balozi Amina Salumu Ali,
alisema wananchi wana kila sababu ya kumchagua Dk. Shein, kutokana na mambo
mengi aliyofanya katika autawala wake.
Aliwataka wananchi wasikubali
kudanganywa na wapinzani badala yake wahakikishe wanakirudisha Chama madarakani
katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Shamsi
Vuai Nahodha, alisema mgombea urais wa chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad,
alikuwa Waziri Kiongozi kwa miaka mine, lakini alishindwa kuibadilisha
Zanzibar, sasa atawezaje kuibadilisha nchi hiyo kwa siku 100.
Alisema mwaka 2010 hadi sasa, Maalim
Seif, alishika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, lakini
ameshindwa kutoa ushauri mzuri ndani ya serikali hivyo aliwataka wananchi
wasikubali kudanganywa na mgombea huyo.
Shamsi ambaye ni Waziri Kiongozi mstaafu
wa Zanzibar, alisema serikali imefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja kujenga Chuo
Kikuu cha Zanzibar, imefanimkiwa kupambana na malaria, kujenga miundombinu ya
barabara na maji na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Balozi Seif Ali Iddi, alisema Maalim
Seif ameishiwa sera na hivi sasa kazi yake ni kueneza uongo kwa wananchi.
Aliwataka wananchi wasikubali maneno
ya uongo wanayoambiwa na Maalim Seif kwani hana uwezo wa kuongoza nchi.
Balozi Idi aliwaomba wananchi
watulie na wasiwe na wasi kwani CCM itashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka
huu.
Alizitaja sababu ya Chama kupata
ushindi kuwa ni pamoja na haijawahi kushindwa, sababu ya kushinda wanayo na
mambo mengi Chama kimefanya.
Hata hivyo, alisema anashangazwa
kuona wapinzani wanataka kujenga ICU Ikulu kutokana na kusimamisha wagombea
ambao ni wagonjwa.
“Mwaka huu tumeshuhudia vioja…mwaka
huu, wapinzani wanataka kuigeuza ikulu kuwa wodi ya ICU kwani Tanzania Bara
wamesimamisha mgonjwa na hapa Zanzibar, mgombea mwenyewe kila sehemu ana
viraka,” alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar,
Vuai Ali Vuai, alisema msingi wa kuingia kwenye uchaguzi ni ilani ya uchaguzi
ambayo tayari CCM, imeshaizundua wakati wa uzinduzi wa kampeni za urais.
Alisema Maalim Seif na wenzake
walizindua kampeni zao bila ya kuwa na ilani ya uchaguzi na kwamba hana jipya
ambalo anaweza kulifanya.
“Maalim Seif ameingia kwenye
uchaguzi bila ya ilani sijui hiyo
serikali ataiongoza vipi,” alihoji.
Vuai alisema baada ya kuona ameingia
kwenye uchaguzi bila ya ilani ya uchaguzi, Maalim alizindua ilani yake juzi
ambayo ina kurasa 94 na kwamba mambo mengi yameyakopiwa kutoka kwenye Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ambayo ina kurasa zaidi ya 236.
Alisema Ilani ya CCM ina sura nane
ambazo kila sura imeelezea mambo ya maendeleo na katika ilani hiyo ya Chama
sura ya kwanza inaelezea masuala ya uchumi na maendeleo.
Vuai alisema nchi zote duniani
huwezi kuwa na maendeleo bila ya amani, uchumi imara, hivyo ipo haja ya
kudumisha Muungano wa Tanzania.
Aliwataka wananchi wakiunge mkono
Chama kutokana na sera mzuri na kudumisha amani iliyopo hapa nchini.
Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu
ya wakazi wa Unguja ambao walifika katika viwanja hivyo kuanzia saa nne,
asubuhi wakiwa na sare za Chama.
No comments:
Post a Comment