Thursday 3 September 2015

UAMINIFU WA MAGUFULI KULIINUA TAIFA-MKAPA




Na Khadija Mussa, Ruangwa
RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amesema uaminifu wa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli,  kiutendaji ndiyo nyenzo pekee itakayoliinua taifa la Tanzania kimaendeleo. 
Pia, ameahidi wakazi wa mikoa ya kusini kwamba atamshawishi Dk. Magufuli kuhakikisha mazao wanayolima kama ufuta na korosho yanaongezwa thamani na kuwa na tija.
Mkapa aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge katika jimbo la Ruangwa ambapo aliwataka wakazi hao kuchagua viongozi wa CCM kwa kuwa ndiyo watakaowaletea maendeleo.
Alisema akiwa rais alifanya kazi na Dk.  Magufuli katika kipindi cha miaka 10 na hata Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi na Magufuli ambaye kwa miaka yote 20 hakuwahi kuonywa wala kulazimishwa kutekeleza majukumu yake na hata ujenzi wa Daraja la Mkapa na kukamilika kwa barabara ya Kibiti - Lindi ni miongoni mwa kazi zake.
Kuhusu mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan,  Mkapa alisema tangu nchi ipate Uhuru haijawahi kuwa na Makamu wa Rais mwanamke, hivyo aliwaomba wananchi hususan kina mama kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuichagua CCM. 
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa, alisema utahakikisha anasimamia na kutekeleza ilani kwa vitendo.
Alisema anaomba wamchague ili waendelee kushirikiana katika kuboresha maendeleo ya jimbo hilo.
Pia, aliwaomba wananchi wasidanganyike na wapinzani wanaopita katika maeneo kwa kuwa hawana dhamira ya dhati ya kutaka kuwaletea maendeleo, hivyo Oktoba 25 itakapofika kura zote kwa wagombea wa CCM.
Kuhusu mgombea urais Dk. Maguli, Majaliwa alisema hana mashaka naye kwa sababu ni viongozi muadilifu, mchapakazi asiyekuwa na kashfa hata moja, hivyo hawana budi kumpigia kura ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi, Mzee Mtopa, aliwataka wanachi kutowapigia kura wapinzani na kwamba mambo yatakuwa poa zaidi wakiichagua CCM kwa kuwa ndicho chama pekee chenye dhamira ya kutaka kuwaletea maendeleo.

No comments:

Post a Comment