Thursday 21 January 2016

BULEMBO AWATANGAZIA VITA WALIMU WAKUU


MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo, amewatangazia vita walimu wakuu wa shule za sekondari zinazomilikiwa na jumuia hiyo na kwamba, wakibainika na ubadhilifu watafukuzwa bila kujali viongozi walioko ndani ya CCM, ambao wamekuwa wakiwakingia vifua na kuwatia jeuri.
Bulembo alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, wakati alipokuwa akifungua kikao cha utendaji kazi cha baraza kuu la jumuia hiyo, kilichowashirikisha walimu wakuu wa shule za jumuiya hiyo pamoja na makatibu wa mikoa wa jumuia.
Alisema hilo litawahusisha pia walimu wakuu,ambao watabainika kutopeleka michango ya wanafunzi wa shule hizo katika ofisi za makao makuu ya jumuia hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema, wapo baadhi ya walimu ambao wamekuwa wakikaidi maelekezo ya jumuia kutokana na kukingiwa vifua na baadhi ya viongozi ndani ya Chama.
"Wakuu wote wa shule za jumuia ya chama wanatakiwa kupelekea michango ya sh. 100,000 makao makuu, ambayo hutolewa na wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza," alisema.
Aliongeza kuwa michango hiyo imeainishwa kwenye fomu za maelekezo ya kujiunga na shule hizo, ambapo tayari wanafunzi hao walishatoa fedha hizo, lakini bado baadhi ya wakuu wa shule hawajapeleka makao makuu.
"Nawasisitiza mpeleke fedha hizo mara moja na endapo agizo hili halitatekelezwa, itabidi waandike barua haraka za kuacha kazi ili tuwaweke pembeni na sheria zichukue mkondo wake," alisema.
Mwenyekiti huyo pia aliwataka wakuu hao wa shule kutofanya kazi zao kwa mazoea, badala yake wawe makini katika utendaji kazi wao kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni za kazi zilizowekwa.
Akisema hivi sasa jumuia hiyo  imekuwa ikifanya ukaguzi wa fedha katika shule hizo na kwamba, walimu watakaobainika kufanya ubadhirifu, watatimuliwa pamoja na kufikishwa mahakamani na kwa wale watakaosalimika wataendelea na kazi.
Mbali na hilo, Bulembo aliwaonya walimu wote wa shule hizo kutofanya siasa mashuleni kwani zimekuwa zikipunguza ufanisi wa kazi kwa walimu.

No comments:

Post a Comment