Saturday, 2 January 2016
SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA BARUA PEPE
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imepiga marufuku matumizi ya barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha wanatumia Mfumo Rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS).
Mfumo huo ulianzishwa na serikali kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia ya mtandao. Waziri wa Nchi, Ofi si ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, wakati akizungumza na watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao.
“Sasa kuna watumishi 7,000 wanaotumia anwani za barua pepe za serikali, idadi hii ni ndogo, lazima iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za serikali kwa kutumia barua pepe nje ya mfumo huu,” alisema.
Hata hivyo alisema serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye mawasiliano binafsi. Alisema kwa kutambua umuhimu wa uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali, ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia barua pepe za serikali.
Angella aliwataka watendaji wa wakala huo kuhakikisha wanasimamia uratibu wa mpango huo, ili wizara, idara na taasisi za umma ziunganishwe na mfumo rasmi wa serikali na kuwa na mfumo mmoja wa mawasiliano. “Katika hili ninatoa siku 60, mhakikishe kuwa mnakamilisha kwa taasisi zilizobaki, ili kwa wale watakaopuuzia hatua zianze kuchukuliwa,” alisisitiza.
Aidha, alitoa wito kwa watendaji wa wakala huo kuweka mpango wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo kazini, kwa kujenga utaratibu wa kuwarithisha uzoefu watumishi ili kuendelea kuimarisha ufanisi na utendaji. Angella aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu katika kuanzisha mifumo mipya ya TEHAMA, ili kuimarisha dhana ya serikali mtandao ili kupunguza gharama hadi kufi kia asilimia tano ya fedha zinazotumika kuendeshea masuala mbalimbali ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA.
Kuhusu ununuzi wa vifaa vya TEHAMA serikalini, waziri huyo aliutaka wakala huo kutoa ushauri ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa, wakati vinaweza kupatikana kwa bei ya kawaida.
Alisema serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma kupitia mtandao, ili wananchi wapate huduma hizo mahali walipo kwa gharama nafuu. Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao, Dk. Jabiri Bakari, alisema umeendelea kupata ufanisi katika uimarishaji wa serikali mtandao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment