Monday 22 May 2017

MAJAJI, MAHAKIMU WATAKIWA KUTENDA HAKI


Na Magreth Kinabo                  

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Ferdinand Wambali, amewataka majaji na mahakimu, kuzingatia maadili ya uhakimu na utumishi wa umma na kutenda haki wakati wanapotimiza majukumu yao.

Aidha, Jaji Wambali amesema, majaji na mahakimu wanapotimiza majukumu yao, wanapaswa kuzingatia kanuni za utendaji wao na za utumishi wa umma, hatua ambayo itawafanya kukidhi matakwa ya wananchi wanaowahudumia.

Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na baadhi ya majaji na mahakimu, katika kikao  kilichofanyika mwishoni mwa wiki, kwenye ukumbi mdogo wa bunge, ulioko jijini Dar es Salaam.

“Suala la maadili lilianza tangu enzi za kale. Jamii ilikuwa inajiwekea maadili. Uwepo wa maadili ni heshima na utii, tabia ya uaminifu, uwajibikaji na kufuata utaratibu kila unapotekeleza kazi,” alisisitiza Jaji Kiongozi.

Alisema kuwa, masuala hayo yalishazungumzwa na kusisitizwa na baadhi ya viongozi wa kitaifa, akiwemo Baba wa Taifa, mwaka 1984 na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mwaka 2011.

Aliongeza kuwa, suala la maadili ni muhimu katika kupambana na rushwa na pia linamfanya jaji au hakimu awe na tabia njema mbele ya jamii, hivyo kazi hizo zinahitaji uadilifu na mtu mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Beatrice Mutungi, akifungua kikao hicho, alisema kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili changamoto za kada hizo na kubadilishana uzoefu wakati wa kutatua changamoto hizo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na baadhi ya viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment