Monday 22 May 2017

WANA-CCM WATAKIWA KUPAZA SAUTI KUWAKATAA WASALITI WATAKAOGOMBEA UONGOZI


WANACHAMA wa  Chama  Cha Mapinduzi  (CCM) mkoa wa Shinyanga, wametakiwa kupaza sauti zao watakapoona viongozi wanawakumbatia wasaliti, ambao watagombea nafasi za uongozi ndani ya Chama.

Katibu wa CCM mkoani hapa, Haula Kachwamba, alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa ziara yake katika wilaya za Shinyanga na Kishapu, za kukagua shughuli za uchaguzi na kutoa semina kuhusu hotuba ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Rais Dk. John Magufuli, aliyotoa Machi, mwaka huu.

Alisema wanachama wa CCM wanayo haki ya kufahamu kuwa, viongozi wao ni wasafi au la,  hivyo aliwataka kutowachagua wasaliti na watoa rushwa, kwani wengi wao huwa ni mapandikizi na sio wanachama safi, hivyo watakwamisha utekelezaji wa Ilani.

“Mkiona viongozi wenu wanawakumbatia wasaliti au watoa rushwa, wakataeni. Mkiona hakuna kinachofanyika, pazeni sauti ili Chama ngazi zingine zijue hapo kuna tatizo,”alisema.

Katika ziara hiyo, Kachwamba alikutana na madiwani, kamati za siasa za wilaya, sekaretarieti za wilaya na makatibu wa Chama wa kata, ambao ni wakurugenzi wa uchaguzi wa kata.

Aliwatahadharisha viongozi hao juu ya athari za rushwa na kupanga safu,  jinsi zinavyokiathiri Chama kwa kupata viongozi wasaliti na wasio na tija na Chama.

“Hotuba ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, aliyoitoa Machi 12, mwaka huu, huko  Dodoma, aliwataka wana-CCM kuacha mazoea ya kuomba na kutoa rushwa katika chaguzi zake na pia kupanga safu na kuwataka kuwa makini,“alisema.

Pia, aliwataka viongozi katika vikao vya uteuzi, kutopitisha majina ya wasaliti na kwamba, majina yao yapo na hata yakipita, hayatarudi, hivyo wasijisumbue.

Katibu huyo alitoa onyo kwa mtendaji yeyote wa Chama katika mko huo, atakayepatikana na tatizo la kuhujumu maagizo ya CCM na kusababisha yote yaliyokataliwa yajitokeze, atawajibika au ajiuzulu mwenyewe.

No comments:

Post a Comment