Thursday 18 May 2017

WANAOTAKA CCM IVUNJIKE HAWATAFANIKIWA


WANAOTAKA Chama Cha Mapinduzi(CCM), kigawanyike vipande vipande kwa sababu ya tamaa ya madaraka na kwa maslahi binafsi, hawatafanikiwa kwenye awamu hii ya Dk. John Magufuli.

Naibu Katibu wa CCM (Bara) ,Rodrick  Mpogolo, aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa majimbo ya Ilala na Kigamboni, katika ziara ya kuimarisha Chama.

Mpogolo alisema wapo watu wanaojipanga kuweka mitandao yao kwenye uchaguzi huu ili waje kuwasaidia watakapogombea ubunge na udiwani mwaka 2020, jambo ambalo halikisaidii Chama.

Alisema CCM haiwezi kukubali mtu mwenye ndoto hizo kutimiza azma yake,
badala yake akigundulika, atatoswa mapema ili Chama kivuke salama kwenye uchaguzi.

"Kiongozi anayepatikana kwa hila, hawezi kuwaunganisha wanachama. Nawaomba watendaji wangu muwe makini na watu hawa maana mkienda kinyume, hatutasita kuwaondoa,"alisema.

Mpogolo alisema mageuzi ndani ya Chama juu ya suala ya rushwa ,kupata uongozi kwa hila ni miongoni mwa mambo yanayopigwa vita kwa nguvu kubwa, hivyo mwanachama atakayethubutu hatapona.

Alisema kuna watu wanajifanya wakubwa ndani ya Chama, ambao wanawajeruhi wanachama wenzao, wanawaumiza na kuwafunga minyororo wengine kwa sababu ya makundi yao.

Aliwataka wanachama wa CCM, watendaji na viongozi, kufanya mabadiliko ndani ya nafsi zao na kamwe wasikubali kuishi kwenye chuki, fitina na makundi ambayo ni hatari kwa Chama.

Aliwaonya wanachama wanaofanya maandalizi ya kuwania uongozi kwa kutegemea kuhonga wapigakura, wasithubutu kufanya hivyo maana watafilisika na uongozi hawatapata.

"Katika kusimamia haki, sitamuogopa mtu yeyote.Watendaji wa jumuia nawaomba msikubali kuvunja miiko na kanuni hata mkipewa maelekezo na makatibu wakuu wa jumuiya.

"Mtendaji atakayejihusisha na kupanga safu, tutamuondoa na kuweka mwingine, maana kuna wanachama wengi wenye uwezo wa kufanyakazi kwa uadilifu,"alisema.

Mpogolo aliwataka wanachama kujenga upendo miongoni mwao na kuwa vishawishi ili kuwavutia wengine wajiunge na CCM, badala ya kununa na kuwa watu wa makundi.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Kusilawe, alisema ziara ya Mpogolo itasaidia kuondoa mapepo ya kuchukiana, makundi na kuwabadilisha wanachama na viongozi.

Awali, akitoa taarifa yaChama, Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Joyce Mkaugala, alisema wamekamilisha uchaguzi kwenye mashina na kwamba, wamepunguza idadi kulingana na mabadiliko ya katiba yanayotaka shina liwe na wanachama 50 hadi 150.

Joyce alisema awali walikuwa na mashina 6,753, lakini sasa yamepunguzwa hadi 3,231 .Alisema wamejipanga vizuri kwenye uchaguzi wa ngazi za matawi.

Katibu huyo pia alimkabidhi naibu katibu mkuu nyaraka mbalimbali zinazohusu vitega uchumi vya Chama, ambavyo vina changamoto ili wasaidiwe katika kuzikabili.

No comments:

Post a Comment